AN-NUUR 
Na.184 Ramadhan 1419, Januari 15 - 21, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Jengo la Waislamu Moshi lageuzwa Kanisa la Walokole 
 
Na Mwandishi Wetu, Moshi
 
  • Bakwata yadaiwa kukatiwa posho
  • Waumini waandaa bakora
IMEDAIWA kwamba jengo la Waislamu lililopo katika shule ya Msingi Mwenge limeuzwa bila ya ridhaa wala kutolewa taarifa kwa kamati husika za Bakwata Mkoa. 

Habari zilizotolewa na kiongozi mmoja wa Bakwata wilaya zimedai kwamba jengo hilo limeuzwa kwa jumla ya shilingi milioni nane. 

Aidha, kiongozi huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini amedai kwamba mauzo hayo yamefanywa na Katibu wa Mkoa Bw. Rashid Malya bila ya kuishirikisha ofisi. 

Jengo hilo ambalo lilirithiwa na Waislamu toka kwa EAMWS lilikuwa likitumika kwa shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na mikutano pamoja na ofisi za Bakwata Wilaya. 

Kwa sasa jengo hilo limekuwa likitumiwa na Walokole kama Kanisa ambapo huendesha kwaya zao. 

Ijumaa iliyopita aliyewahi kuwa Katibu wa Bakwata Mkoani Kilimanjaro Alhaj Omar Sinare alilaani vikali kuuzwa kwa jengo hilo kinyemela na kugeuzwa Kanisa lisilo rasmi. 

Alhaj Sinare akiungwa mkono na mamia ya waumini walioswali katika Msikiti wa Riadha alimtaka Sheikh wa Mkoa na Katibu wake kuwapa Waislamu maelezo ya kutosha kuhusu amana zao. 

Habari zaidi zimeeleza kwamba imeteuliwa Kamati ambayo itafuatilia suala hilo na Bw. Malya ametakiwa atoe taarifa ya kueleweka kwa kipindi cha wiki moja. 

Baadhi ya waumini walioongea na mwandishi wa habari hizi, wamedai kwamba wanachofanya hivi sasa ni kuandaa bakora zao huku wakisubiri taarifa ya Kamati. 

Wamesema kwamba hawatavumilia kuona Walokole wakiimba ndani ya jengo lao au kuuzwa kwa yoyote wala hawatamvumilia Bw. Malya kama wakati ule alivyouza gari la ofisi. 

Taarifa kamili itakayoamua matumizi ya bakora hizo imedaiwa kwamba itatolewa (leo) Ijumaa baada ya swala katika Msikiti wa Riadha. 



Masjid Nurania yaswaliwa Ijumaa 
 
  • Watakiwa kutofanya Misikiti magofu
  • Kina mama waonyesha vazi la Hijab linavyotumika
Na Rajab Rajab, Morogoro
  

HATIMAYE Msikiti wa Nurania uliopo eneo la MODECO mjini hapa umeamua rasmi kuswaliwa swala ya Ijumaa tangu kufunguliwa kwake mwezi Novemba mwaka jana. Msikiti huo una uwezo wa kuswaliwa zaidi ya watu mia moja. 

Ufunguzi wa Msikiti huo uliofanyika Ijumaa iliyopita ulizinduliwa rasmi kwa kusomwa Qur’an kutoka kwa Sheikh Abu Twalib Mohammed kutoka Misri. 

Pia ilifuatiwa na hotuba na mawaidha kutoka kwa Sheikh Ibrahim Mohammed ambaye ni mwalimu wa Chuo cha Markaz cha Jijini Dar es Salaam. 

Katika hotuba yake, Sheikh Ibrahim Mohammed amewaeleza Waislamu kwamba kuna faida kubwa sana kwa mtu kujenga au kuchangia ujenzi wa Msikiti, ambapo amesema hiyo ni sadaka yenye kuendelea kumpata mtu mpaka Msikiti huo utakapobomoka. 

Sheikh Mohammed ambaye alikuwa akiongea kwa lugha ya Kiarabu na kukalimaniwa na Ustadh Ally Omar Ngalawa, amezitaja sadaka zingine zenye kuendelea na ambazo amewataka Waislamu wajitahidi kujihusisha nazo ikiwa ni pamoja na kujenga visima, madrasa pamoja na kutengeneza barabara. 

Aidha, Sheikh huyo amewataka waumini wa Msikiti huo kutumia Msikiti huo katika nyakati zote tano za swala na amewaasa kutoufanya gofu kwa kwenda kuswali mpaka itokee sherehe za Iddi au Ijumaa kama ile. 

"Mwenyezi Mungu amesema katika majumba kuna majumba ambayo anataka kutajwe Yeye na kutukuzwa tu na majumba hayo si mengine bali ni Misikiti", amesema. 

Wakati huo huo, Changamoto imetolewa kwa kina mama wa mkoa huu na nchi kwa ujumla kujisitiri maungo yao kwa kuvaa hijab ambalo ndilo vazi linalotakiwa kuvaliwa na mwanamke wa Kiislamu mahali popote duniani. 

Changamoto hiyo imetolewa Jumamosi iliyopita wakati wa mhadhara wa kina mama uliofanyika katika Msikiti wa Mafiga kwa lengo la kukazia lengo na umuhimu wa swaumu pamoja na vazi la hijab ambapo akina mama hao waliweza kuonyesha vazi hilo linavyoweza kuvaliwa katika shughuli mbalimbali za kina mama kama vile kupika, kuchota maji, kwenda sokoni na hata katika kazi za kulima. 

Aidha, katika mhadhara huo uliohudhuriwa na wanawake mbalimbali wa mkoa wa huu ambapo mgeni mwalikwa alikuwa Bi. Khadija Muharam ambaye ni Mwenyekiti wa wanafunzi mjini Iringa, wanawake nchini kote wametakiwa kujitahidi kadri ya uwezo wao kuweza kufikia lengo lafunga ambalo ni kuwa wacha Mungu na kujenga familia za Kiislamu katika jamii zao kwa kuzingatia kuwa mama ana nafasi kubwa sana ya kuweza kujenga familia bora kutokana na ukaribu wake na familia. 

Pia wanawake hao katika mhadhara wao huo, waliwaomba Masheikh na walimu wengine kujitahidi kuwaelimisha Waislamu katika mwezi huu mtukufu, waweze kuwa wengi na hata katika miezi mingine ili kuweza kuimarisha dini ya Mwenyezi Mungu ambayo amewachagulia waja wake (Uislamu) kama ndiyo dini yao. 



Jabal Hira kutoa mafunzo ya Kompyuta Morogoro 
 
  • Itaanza kwa wanafunzi wa Kidato cha IV hadi cha VI
Rajab Rajab na Mussa Ally, Morogoro

TAASISI kongwe ya Kiislamu Jabal Hira ya mjini hapa imeazimia kuanza kufunza maarifa ya Kompyuta katika siku chache za usoni ili kuwawezesha Waislamu wa Morogoro kuingia katika karne ya sayansi na teknolojia kifua mbele. 

Akizungumza katika sherehe fupi za kumuaga mfanyakazi wa siku nyingi wa taasisi hiyo, Bw. Abdallah Suleiman aliyestaafu baada ya kuitumikia kwa miaka 16 mfululizo, kwenye ofisi za sekondari ya Jabal Hira mwishoni mwa wiki, Mkuu wa Shule hiyo Bw. Nasser Shaweji alisema kuwa maandalizi ya kwanza kwa mpango huo ikiwa ni pamoja na chumba maalum, samani, vifaa vya kufundishia na walimu tayari vimekwishakamilika. 

Alisema kwamba kwa kuanzia, wanafunzi wa kidato cha nne, tano na sita watafaidika na mpango huo kwa mwaka huu, kabla haujasambazwa shule nzima. 

Aidha, Waislamu wa mjini Morogoro watafaidika na mpango huo, kwani yatatolewa masomo ya jioni ya fani hiyo ambapo walimu kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) wa mjini hapa watatoa mafunzo hayo. 

Mapema katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Shule hiyo alitoa zawadi ya baiskeli yenye thamani ya zaidi ya shilingi 70,000 kwa Bw. Abdallah Suleiman aliyestaafu mwishoni mwa mwaka jana. 

Akitoa nasaha zake, Mwenyekiti huyo Bw. Kassim Kivuli alimsifu Bw. Abdallah kwa uwajibikaji wake na uaminifu, sifa ambazo mfanyakazi wa Kiislamu anatakiwa awe nazo. 

"Uaminifu wake na uwajibikaji wake kwa mwajiri wake unatosha kuwa mfano wa kuigwa kwa wafanyakazi wengine", alisema Bw. Kivuli. 
 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
Tahariri 
Baada ya futari nzuri: Tuwatupie macho wenye njaa 

Rais Mkapa kuwa mgeni rasmi Baraza la Idd 

Ubungo yakumbwa na ukame 

Waumini, Masheikh Arusha wasutana kwa futari ya Mrema 

Dondoo za saikolojia 
Na. Abu Halima Sa Changwa 

Waislamu turejee kwa Allah 

MSADAT yazidi kutia moyo Tanga 

Mjue Usama bin Ladin 

MAFUNZO KUHUSU FUNGA YA RAMADHANI 

Michezo isiyoruhusiwa katika Uislamu 

Ustadh Farid: Kijana aliyejitolea kuwapa Da'awa watalii 

Hakuna Magharibi wala Mashariki: Uislamu ni ubinaadamu 
Na Abubakari S. Marwillo 

Ijue madrasati Mar-wa ya Dodoma mjini 
Na Abu Zuberi, Dodoma 

Ijue Madrasat Jadidul Fiqhyyat - Tabata Kimanga 
Na B. Mwakangwale 

Madrasat Hidayatul Muumini Mwadui 

Washindi wa mashindano ya Hadithi za Mtume (s.a.w.) wapatikana 

Madrasa Shafii Ujiji Kigoma yaonyesha umahiri wake 

Waanzisha mifuko kusaidia wagonjwa Dodoma 

Waislamu Kondoa waomba msaada kumalizia Msikiti 

Mnyororo wa imani-2 
Na Sheikh Bernard P. Nyangasa 

Kutoka magazeti ya zamani: 
Wanaoshitakiwa kwa uhaini kortini leo 

Jengo la Waislamu Moshi lageuzwa Kanisa la Walokole 
Na Mwandishi Wetu, Moshi 

Masjid Nurania yaswaliwa Ijumaa 
Na Rajab Rajab, Morogoro 

Jabal Hira kutoa mafunzo ya Kompyuta Morogoro 
Rajab Rajab na Mussa Ally, Morogoro 

Sayansi na Teknolojia 
[Internet ni nini?] 

Masomo ya Dini ya Kiislamu 

Barua za Wasomaji 

Mashairi 

Chakula na lishe 
[Thamani ya mlo wa Uyoga] 
 


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita