Ndugu Mhariri
AWALI ya yote ningependa kumpongeza Mbunge wa Kigamboni Mh. Kitwana Kondo kwa kuwa mkweli na muwazi Bungeni kuhusu dhulma wanazofanyiwa Waislamu. Mh. KK anatetea haki za Waislamu zinazolindwa na katiba. Ni wajibu wetu kumpongeza kwa sababu mambo anayoyazungumza ndiyo msingi hasa wa maelewano yetu na umoja wetu wa kitaifa tunaojivunia. Wala siyo uchochezi kwa maana ya madhalimu. Kukosoa na kuonyesha dhulma kwa lengo la kujenga ni uchochezi unaofaa.
Ama kuhusu hili suala la serikali juu ya hijab mashuleni; ugonjwa uko serikalini kwenyewe. Serikali haiko ‘serious’ na ule waraka unaoruhusu vazi hili mashuleni huenda ulikuwa ni ‘danganya toto’ tu ya kuwafunga Waislamu midomo.
Tangu waraka EDC/10/62/VOL 1/147 utolewe na Kamishna wa Elimu mwaka 1995, suala la hijab mashuleni na vyuoni limekuwa ni ‘agenda’ iliyosahaulika. Lakini nani atasimamia agizo hili halali la serikali! Ngazi zote muhimu wamejaa wenyewe (wachapakazi). Na wana mkakati wa pamoja wa kukwamisha haki hii ya Waislamu.
Katika mazingira ya kawaida, serikali ndiyo mdhibiti mkuu wa mambo yote ya dola. Serikali inapotoa agizo fulani ina wajibu vile vile wa kuhakikisha kwamba agizo hilo linatekelezwa. Ndiyo sababu ya serikali kukabidhiwa vyombo vya dola kama polisi, mahakama, magereza, majeshi kama nyenzo ya kulindia katiba na maagizo halali yatokanayo na katiba hiyo hiyo. Ni udhaifu kwa serikali kuendelea kutoa agizo lile lile wakati utaratibu wa kuwajibishana upo.
Tangu lini agizo halali la Waziri wa Elimu na Utamaduni likapuuzwa na mwalimu wa shule ya msingi! Huyu mwalimu hajui hata bajeti ya mishahara yake kwa mwaka inapitishwa vipi na Mheshimiwa Waziri Bungeni! Sasa hii jeuri iliyopea na utovu wa nidhamu inatoka wapi? Bila shaka ni athari za mfumo mkongwe wa kukandamiza Uislamu na Waislamu uliojengwa katika jamii yetu ndiyo unaoleta kibri. Imefikia mahali hata mwalimu wa UPE anaweza kubishana na Waziri katika jambo la haki za Waislamu na isiwe kitu. Kuna watu wanadhani ni mwiko kwa Waislamu kuishi Kiislamu.
Kusema kwamba hatuwezi kuwaruhusu wanafunzi wa Kiislamu kuvaa hijab kwa sababu hatuna waraka wa serikali unaoelekeza hivyo ni kisingizio dhaifu na kinachoonyesha jinsi baadhi ya walimu wakuu walivyokuwa vipingamizi dhidi ya Uislamu. Kama wangetaka waraka huo wangeupata. Ingekuwa waraka wa mikopo ya Sikukuu au nyongeza ya mishahara basi ingeshapatikana katika mashule yote nchini na ungetekelezwa kwa ustadi mkubwa kabisa. Lakini huu wa hijab nani ataufuatilia!
Msisitizo na ufafanuzi wa Waziri wa Elimu na Utamaduni kuhusu hijab alioutoa bungeni hivi karibuni unaonyesha dhahiri jinsi serikali inavyoshindwa kuwachukulia hatua zinazofaa watendaji wabovu wa serikali wanaokwamisha zoezi hili. Pamoja na nia njema ya serikali, ningependa kumshauri Waziri wa Elimu na Utamaduni atumie madaraka yake kulinda maagizo ya serikali yake mbele ya wabunge na wananchi kwa ujumla kwamba serikali imesharuhusu mabinti Waislamu wavae mavazi yanayolingana na imani yao. Hawa walimu wenye ‘agenda’ ya udini wanajua hatari ya kosa wanalolifanya?
Kwa Waislamu; hawahitaji kulipigania suala hili kwa mara ya pili. Watumie kauli ya Waziri wa Elimu aliyoitoa bungeni kama sababu ya kuwavishia mabinti zao hijab. Kama walimu’ wadini’ hawataki waache kazi. Hizi siyo zama za kunyanyasana wala kubaguana kwa misingi ya kidini. Wakiwafukuza madarasani; basi Waislamu watumie taasisi zao na mabaraza yao kupambana na walimu hawa hata ikibidi shule kufungwa!
Ninamalizia kwa kuitahadharisha serikali ione jinsi tatizo hili linavyochupa mipaka. Hili halihitaji utafiti wa kisayansi kuligudua. Ni kiasi tu cha kuwaona wanafunzi waathirika na walimu wanaohusika. Msisubiri hasira za Waislamu kama ilivyokuwa kwa mabucha ya nguruwe mwaka 1993. Walimu wote wanaohusika na unyanyasaji huu wawajibishwe mara moja kabla mambo hayajaharibika zaidi. Maana kuna baadhi ya watu wamezoea kujifunza kwa njia ngumu. Hawaelewi mpaka wapigwe konzi. Mwalimu gani anayeshindwa kuelewa hatari ya kuzuia haki inayolindwa na katiba!
Bisura Waziri Nyello,
Dar es Salaam.
Ndugu Mhariri
KWA kupitia gazeti lako tukufu ambalo linawapatia walio wengi maadili mema na mambo mengi yahusuyo Akhera na dunia, napenda nitoe pongezi na shukrani kwa dada zetu wa Kiislamu kwa ujasiri waliouonyesha kwa kupitia gazeti hili tukufu kujitoa mhanga kujitangaza kupatiwa (nusra) na vijana wa Kiislamu kwa ni a ya kufunga ndoa. Nawapongeza dada zetu kwani kufanya hivyo ni njia mojawapo ya kuupigania Uislamu kwa kutaraji kupata kizazi chema chenye kufuata maamrisho na makatazo ya Allah (s.w.).
Na kwa kutumia njia hiyo ni rahisi kumpata mke au mume ambaye anaweza kuifunza familia malezi bora na humo tukaweza kupata huko mbeleni wapigania haki (wanaharakati) wa kuutetea Uislamu huko mbeleni.
Mwisho natoa mwito kwa vijana wa Kiislamu wanaotaka kuoa kuiga mwenendo huo ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza baada ya ndoa unaosababishwa na mke au mume ambaye hajui maamrisho au makatazo ya Allah (s.w.)
Murshidu Issa,
P.O.Box 3418,
Dodoma.
Ndugu Mhariri
WAKATI huu ambapo Tanzania imo katika mjadala wa utungaji wa katiba mpya, moja ya suala linalowagusa sana wananchi ni hatma ya Muungano.
Watu lazima wakumbuke kwamba "Articles of Union" ziliainisha mambo 11 tu, ambayo kama kuna ridhaa, ridhaa hiyo ya Muungano wa Watanganyika na Wazanzibari basi uliishia juu ya hayo mambo 11 na kutoa mamlaka kwa Bunge kutungia sheria na kusimamia utekelezaji wake Kimuungano kama kifungu (iv) cha "Article of Union" kinavyoonyesha. Ajabu kubwa ni kwamba leo mambo ya Muungano ni 22 badala ya 11, hapana shaka upande mmoja wa Muungano una haki kamili ya kuhoji uhalali wa mambo 11 ya nyongeza.
Kwa vile Bunge la Jamhuri ya Tanzania lilishiriki kikamilifu katika uongezaji huu ni sawa kuliuliza lilipata wapi ridhaa ya wananchi? Bunge la Tanzania ni la kutunga sheria (Legislative Assembly) na sio bunge la kikatiba (Constituent Assembly), leo iweje likurupuke na kuwatungia watu katiba au kwanini mambo 11 ya awali yahitaji ridhaa na mikataba lakini mambo 11 ya nyongeza yaingizwe kinyemela ndani ya Muungano pasi na ridhaa ya wananchi.
Kuna ushahidi wa wazi kabisa kwamba upande fulani wa Muungano haukuridhika na ufanywaji wa "dhambi" hii na walihoji uhalali wa uongezwaji wa mambo ya Muungano toka 11 hadi 22 mwaka 1977 na mpaka kutaka kufikisha shauri lao katika mahakama ya katiba, lakini watendaji dhambi walifanya mizengwe na kuwafukuza madarakani mkoani Dodoma mwaka 1984. Mbegu ya kwanza ya mfarakano hapo ikapandwa.
Kwa vile ndio iliyokuwa ukiritimba wakati huo basi kama kawaida yake haikuacha kujitoa kimasomaso "dhambi" hii kubwa wakiita kasoro za Muungano. Na Tume mbalimbali zikaundwa chini ya Dk. Salmin Amour, Ndg E.M. Mtei, Mh. F.L. Nyalali na Mh. W. H. Shellukindo ili kuondoa hizi kasoro ambazo hadi leo bado zinaongezeka tu.
Lakini kwa bahati nzuri au mbaya wakati uchaguzi wa 2000 unakaribia, mzozo wa Zanzibar unafukuta na Katiba ya sasa kushindwa kukidhi mahitaji, ule ufa uliozibwa kwa kifimbo badala ya kipande cha chuma sasa unaelekea kuvunja ukuta mzima.
Shoka bin Shamte,
Pemba- Zanzibar.
NAOMBA unipe nafasi katika safu ya barua zetu ili kuwaweka sawa wale wote wanaodai kuwa 1998 ilimalizika kwa amani Tanzania.
Ukweli ni kuwa 1998 haukuwa mwaka wa amani, bali utulivu wa wananchi, kuuheshimu utu wao; kwani wengi wanadhani amani inatoweka pale patakapotokea vita kama vile Congo au kiongozi fulani wa nchi kuuawa.
Ninasema hivyo, sababu kuna matukio mengi yaliyopelekea kuhatarisha amani nchini na kutoweka.
Mauaji yaliyofanywa na polisi kule Mwembechai bila ya watuhumiwa kuchukuliwa hatua. Vitisho vinavyofanywa na polisi, vilivyofanya watu wengine kuishi bila viungo vyao, nani wa kulaumiwa?
Mlipuko wa mabomu ubalozi wa Marekani nchi yenye amani, milipuko haiwezi kusikika, ambapo watu walipoteza maisha yao.
Rushwa imepelekea kuondoa haki katika taifa na kilichobaki ni kuvumiliana. Hukumu zinatolewa zinategemea rushwa.
Watanzania wenzetu wanateseka gerezani kule Zanzibar mpaka leo mashitaka hayajawekwa wazi. Serikali kuwa radhi na mateso hayo.
Kutokuwepo kwa huduma za kijamii, kama maji, watu hufa kwa njaa na wahusika kukanusha vifo vinavyotokea, madawa na kupandishwa kwa huduma mbalimbali kutokana na VAT.
Ubinafsishaji ambao utatupelekea kutawaliwa kisaikolojia na wale waliotupatia uhuru 1961 na kuwafanya viongozi wetu kuwa vibaraka wa mali zao, huku Watanzania tunaendelea kufa, kuandaa semina na ziara nchi za nje.
Uwekezaji katika uuzaji na ununuzi silaha hautakuwa nahaki na usawa, wanachi wasiokuwa na uwezo wa silaha watauwawa bila kupata mtetezi na upekuzi wa balozi kwa balozi utaongezeka.
Viongozi wanaoendelea kututangazia mali zao wasije wachochea watu wawaandalie matairi na petroli kuwachoma moto kwa kudhaniwa ni vibaka, sababu wanakuwa wababaishaji na upatikanaji wa mali zao wakati wapiga kura wanakufa kwa njaa na kula mizizi, hawataki amani iwepo nchini.
Kuna matukio mengi kama haya yaliyohatarisha na kutoweka amani mwaka 1998 wananchi wakaachwa wakivumilia huku wakiliwazwa na maneno ya jukwaani. Kwa hivyo Tanzania kuna utulivu na sio amani.
Mpenda amani,
Mohamed Amir, Mchomvu,
Dar es Salaam.
|
|