Na Mjahid Mwinyimvua
GAZETI la Mtanzania la Februari 20, mwaka huu limeripoti kuwa Mahakama ya Jiji (Dar es Salaam) imekifungia kiwanda cha kutengeneza maji ya kunywa ya Best Drinking na cha kuoka mikate cha Afri kwa kukiuka sheria za udhibiti wa vyakula na dawa na kuendesha biashara bila ya kuwa na leseni.
Gazeti hilo linaendelea kulipoti kuwa "Hakimu Fatuma Kiwanga aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, alimhukumu Meneja wa kiwanda hicho, Chrysostom Mwakalinga kulipa faini ya shilingi 30,000 baada ya kukiri makosa. Hata hivyo, Hakimu Kiwanga alisema kuwa kiwanda kicho kitaruhusiwa kuendelea na uzalishaji baada ya kukamilisha mambo yote yanayotakiwa kulingana na sheria za uthibiti wa chakula.
Vile vile gazeti hilo limeripoti kuwa "makosa mengine yaliyosomwa mahakamani hapo dhidi ya washitakiwa ni wafanyakazi kufanya kazi bila ya kupimwa afya zao na kutokuwa na sare".
Zaidi ya hayo, gazeti hilo la Mtanzania liliripoti kuwa, "mahakama hiyo (ya jiji) imekifungia kiwanda cha kutengeneza mikate cha Afri Bakery Dar es Salaam baada ya kukitia hatiani kwa kukiuka kanuni za afya kwa kuendesha biashara bila ya leseni.
Akisoma shitaka dhidi ya Meneja wa kiwanda hicho Atul Sheth, Mwendesha mashitaka Kuoka alidai kuwa maofisa wa afya wa Tume ya Jiji walikikuta kiwanda hicho kikifanya kazi bila ya kuwa na leseni kutoka Tume ya Taifa ya Uthibiti wa Chakula. Meneja huyo alihukumiwa kutumikia kifungo cha miezi minne jela au kulipa faini ya shilingi 40,000. Alilipa faini hiyo", mwisho wa kunukuu.
Nimenukuu sehemu kubwa ya habari hii katika gazeti ili wasomaji wangu waweze kufuatiila vizuri makala yangu.
Kabla ya kutazama ni kwa vipi serikali inavyofanya mchezo na uhai wa raia wake, ni vyema kwanza nikafanya uchambuzi wa habari niliyoinukuu hapo juu.
Kuzalisha chakula bila leseni
Inaposemwa kwamba kampuni au mtu fulani anazalisha na kuuza maji ya kunywa, mikate au chakula chochote hasa katika viwanda bila ya leseni, maana yake ni kuwa mfanyabiashara huyu anazalisha na kuuza chakula (au majiý) bila ya chakula (au maji) hicho kuthibitishwa kama kinafaa kwa matumizi ya binadamu au la, na vyombo vya serikali.
Na kwa vile mfanyabiashara huyu si muaminifu (amekwe;pa leseni) kuna uwezekano mkubwa kuwa anazalisha chakula kisichofaa kwa matumizi ya binadamu. Hivyo, kosa hilo si jepesi kama wengi wanavyodhani.
Yaani, tatizo siyo kutokuwa na leseni bali ni kuzalisha chakula ambacho kinaweza kudhuru afya na hatimaye kuleta madhara kama utaahira, utasa au hata kifo kwa watumiaji wa chakula hicho.
Afya na sare za wafanyakazi
Wafanyakazi hasa katika viwanda vya vyakula na katika mahoteli lazima wapimwe afya zao kama sheria inavyosema vinginevyo, wale wagonjwa wanaweza kukichafua chakula na hatimaye walaji wanaweza kupata maradhi.
Sare za wafanyakazi pia zinafaida kubwa katika kiwanda kama cha kutengeneza chakula.
Adhabu waliopewa wahalifu
Baada ya uchambuzi wa hapo juu ni matarajio yangu kuwa wasomaji wangu mmeona ukubwa wa kosa la hao walalifu na watu ambao ni hatari kwa maisha yetu.
Hata hivyo, nina imani kuwa mmesikitishwa na adhabu waliopewa watu ambao wanaweza kusababisha madhara makubwa katika jamii.
Hapa ni vyema pia mkakumbuka kuwa maji ya kunywa na vyakula ni vyanzo vikubwa vya maradhi kama vile kipindupindu, homa ya matumbo, kuharisha, n.k. Magonjwa hayo kama tunavyojua yanateketeza mamia ya roho za Watanzania kila mwaka.
Cha ajabu kama nilivyosema awali kuwa ile adhabu anayopewa mfanyabiashara mhalifu ya shilingi elfu therathini au elfu arobaini au kifungo cha mieazi minne!
Elfu thelathini au arobaini ni kitu gani kwa mfanyabiashara mwenye kiwanda (siyo mama ntilie) ? Ama kweli serikali inafanya mchezo na roho za wananchi wake. Sijui wakitoweka nani ataepiga kura au nchi itakwenda na viongozi pekee bila raia!
Namna serikali inavyohusika katika kadhia hii
Kama tunavyojua mahakama ya Jiji au yoyote ile kwa namna fulani ipo chini ya serikali kuu. Hivyo, haiwezi ikafanya kinyume cha sheria mama (Katiba) na ikaachwa. Katiba imeahidi kulinda uhai wa Watanzania. Lakini, wafanyabiashara wachache wanahatarisha uhai wa Watanzania na wageni pia.
Serikali kuu iko kimya. Lakini hiyo hiyo ndiyo iliyoivunja Halmashauri ya Jiji (Dar es Salaam) na kuunda Tume ya Jiji. Ambayo leo mahakama yake inatoa faini ya elfu thelathini na kuahidi kutoa ruhusa y akuzalisha tena bidhaa kwa mfanyabiashara aliyeonyesha tabia ya udanganyifu!
Kwa kupitia makala hii, nasisitiza kuwa serikali
kuu iache kufanya mchezo wa uhai na raia wake na ifanye hima kuweka mambo
sawa katika mahakama ya Jiji kama ilivyofanya hima kuweka sawa marupurupu
ya waku wa waliostaafu na wale watakaostaafu.
|
|