Madai ya kumsaka Ponda:
Wananchi walaani matamshi ya Ameir
 

WANANCHI sehemu mbalimbali nchini wamelaani matamshi ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Bwana Ali Ameir kwamba polisi itaendelea kumsaka Sheikh Ponda hata kwa miaka kumi ijayo ili ajibu ‘shitaka’ la kuhusika na vurugu zilizotokea Mwembechai.

Wananchi hao wamemtaka Bwana Ali Ameir kuacha propaganda za kufunika ukweli kuhusiana na mauaji ya Mwembechai. Matamshi ya Bwana Ali Ameir yaliripotiwa na gazeti moja binafsi litokalo kila Jumapili.

Akizungumza na waandishi wa gazeti hilo waliokwenda ofisi kwake kutaka kauli kuhusiana na madai ya polisi kumsaka Sheikh Ponda, Mh. Ali Ameir ameripotiwa kudai kwamba serikali itaendelea kumsaka Sheikh huyo kwa kile alichodai kuhusika kwake na vurugu za Mwembechai ambazo zilisababisha mauaji ambayo serikali hivi sasa inalaumiwa kutoka kila kona.

Wananchi wengi waliopata fursa kutoa maoni yao kufuatia matamshi ya Waziri Ameir wamemshutumu Waziri huyo kwa ufunikaji wa ukweli na kutokuwa makini katika uzungumzaji.

Akitoa maoni yake Bwana Rajab Hambalize wa Vingunguti Jijini alitaja moja ya kauli ya Mh. Ameir zilizozua tafrani kwamba ni ile ya kuzihusisha baadhi ya nchi na kadhia za Mwembechai kauli ambayo ilisababisha baadhi ya balozi kutaka ufafanuzi vinginevyo zingevunja uhusiano na Tanzania.

Bwana Lucas Faibe wa Ubungo alimshangaa Bwana Ali Ameir kwa kutochukua hatua ya kujiuzulu hadi hii leo kutokana na kashfa ya mauaji ya Mwembechai.

Mkazi huyo wa Ubungo alidai kwamba Bwana Ali Ameir ni mmoja wa wahusika wakuu wa kadhia hiyo ambao alidai kama serikali ingekuwa yenye kujali hisia za wananchi wake ingewawajibisha na kuwachukulia hatua za kisheria.

Naye Bi Fatuma Musa mkazi wa Mwananyamala Jijini aliliambia gazeti hili kuwa alichofanya Mh. Ali Ameir katika matamshi yake ni kujaribu kujenga hali ambayo itafanya lisahaulike suala la msingi badala yake lijadiliwe suala jingine.

"Anachofanya Mh. Waziri ni kuhamisha mjadala hatua itakayopelekea kusahauliwa suala husika", alisema Bi Fatma.

Bwana Hassan Maleba wa Dodoma akiongea kwa njia ya simu na gazeti hili, alihoji sababu ya kukaidi kwa serikali kuunda tume huru kuchunguza suala la Mwembechai.

Alisema kuundwa kwa tume hiyo kungewezesha kujulikana kiini cha suala hilo sambamba na kuwajua wahusika wakuu wa kadhia hiyo iliyopelekea polisi kuua Wananchi wasio na hatia.

Naye Mwandishi Wetu kutoka Mwanza anaripoti makundi ya watu mjini humo yamekuwa yakiongelea matamshi ya Waziri Ameir kwa kuhoji ahadi ya Rais Benjamin Mkapa kuhusu kutafuta kwake ushahidi wa kisayansi juu ya malalamiko ya Waislamu.

Wananchi mbalimbali mjini Mwanza wameonyesha kusikitishwa na jinsi viongozi wasivyokuwa na utaratibu mzuri wa utoaji wa kauli za serikali.

Wananchi kadhaa mjini humo wameonyesha kupingana kwa kauli zinazotolewa na viongozi wa juu wa serikali ambapo Rais aliahidi kushughulikia madai ya Waislamu likiwemo la Mwembechai, Waziri Mkuu akayapa unyeti madai hayo kiasi cha kuzuiwa kujadiliwa bungeni , Makamu wa Rais akaibuka na kauli ya kupinga na kuyaita ya uongo.

"Katika hali hii, kiongozi huyu anasema hili na yule anasema lile, wananchi tukamate la nani?", wamehoji watu wengi waliohojiwa na gazeti hili.

Kutoka Kigoma Ibrahim Magala anaripoti kuwa Waislamu mkoani humo wako katika maandalizi ya kuwasilisha salamu zao kwa Rais kupitia Mkuu wa Mkoa huo.

Kuhusiana na matamshi ya Waziri Ameir, Wananchi wa Kigoma wamesema kwamba imekuwa ni kawaida kwa viongozi wa Wizara hiyo kutafuta visingizio visivyo na msingi kuhalalisha dhuluma dhidi ya Waislamu.

Wamesema kabla ya Waziri aliyepo sasa, walipita Mawaziri waliopata kuzifuta jumuiya halali za Waislamu, wapo waliowasingizia Waislamu kuingiza makontena ya majambia ili wafyeke shingo za Wakristo na wako waliowaweka rumande Waislamu kwa madai ya uongo na hata kuwafunga.

Wakati akifunga mjadala wa Wizara yake katika kikao kimoja cha Bunge, Waziri wa Mambo ya Ndani Mh. Ali Ameir alipata kutamka kwamba sababu ya mtoto Chuki Athumani kupigwa risasi na polisi ilikuwa ni kukutwa na makaratasi ya uchochezi.

Hata hivyo, Mheshimiwa Ameir hakuweza kufafanua iwapo mtoto huyo alipigwa risasi kabla au baada ya kukutwa na makaratasi hayo.
-

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook