Uendeshaji wa Mashitaka - 4
Kusoma Shitaka na Majibu
 

SIKU ambayo kesi inaanza dhidi ya mshitakiwa ni lazima asomewe shitaka analokabiliwa nalo (F.228. Sheria ya Mwenendo wa Jinai. I.h.j). Ni lazima mshitakiwa awepo mwenyewe mahakamani kujibu shitaka na kusikiliza ushihidi dhidi yake (F.196. Sheria ya Mwenendo wa Jinai. I.h.j) isipokuwa kama anaumwa anawakilishwa na wakili (F.197(B), Sheria ya Mwenendo wa Jinai. I.h.j). Anaweza pia asitakiwe kuwapo mahakamani ikiwa kuwepo kwake kunaingilia uendeshaji wa shauri hilo. (F.197(A), Sheria ya Mwenendo wa Jinai. I.h.j).

Katika shauri la Wachira Murage v. R. (1956 23 E.A.C.A. 562) mshitakiwa, ambaye alikuwa amekabiliwa na shitaka la mauaji ya kukusudia, alikataa kujibu shitaka la mauaji. Jaji aliandika kuwa mshitakiwa huyo amekana shitaka. Lakini mshitakiwa aliendelea kufanya fujo wakati wa kusikiliza shauri hilo ikawa vigumu kuzikilizana. Taarifa ya daktari ilionyesha kuwa mshitakiwa alijisingizia lakini hakuwa kichaa. Hivyo Jaji aliamuru mshitakiwa atolewe nje ya mahakama, akawa anapelekwa mahakamani kutambuliwa tu, kutoa ushahidi wake, na mwisho kusomewa hukumu na adhabu yake.

Ni makosa kumtoa mahakamani mshitakiwa katika hatua yoyote ile isipokuwa kama mwenyewe amefanya fujo. Mathalan katika shauri la George Smelli (14 Cr. App. R. 128) mahakama yaliamuru mshitakiwa atolewe nje wakati binti yake anatoa ushahidi. Mshitakiwa huyo alitolewa na kuwekwa nje ya jengo la mahakama ambapo angeweza kusikia ushahidi uliokuwa ukitolewa na binti yake ambaye ilidaiwa alimshambulia na kutompa matunzo mazuri. Mahakama hayo yaliona kuwa binti huyo angetishika kama mshitakiwa angebaki mahakamani. Mahakama ya Rufani yalisema ilikuwa ni makosa kumtoa mshitakiwa nje wakati binti yake anatoa ushahidi. Yalidai kuwa kuwepo kwa mshitakiwa kungesaidia binti yake kusema kweli. Hivyo yalibatilisha uamuzi wa mahakama ya awali dhidi ya mshitakiwa.

Shitaka litasomwa na mahakama yenyewe yaani Hakimu au Karani wa Mahakama. (F.228(1), Sheria ya Mwenendo wa Jinai. I.h.j). Na sehemu zote mbili: Maelezo ya shitaka pamoja na muhtasari wake lazima kusomwa.

Kuna aina nne kuu za majibu ya shitaka: Kuungama shitaka, (F.228(3). Sheria ya Mwenendo ya Jinai. I.h.j), kukana shitaka (F.228(2). Sheria ya Mwenendo ya Jinai. I.h.j),

kutoa hoja kwamba mashitaka ni batili kwa vile tayari mshitakiwa alihukumiwa akaachiwa au kutiwa hatiani kuhusiana na mashitaka hayo hayo; (F.137. Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j), mwisho, kutoa hoja kwamba mahakama yanayotaka kusikiliza shauri hilo hayana mamlaka ya kufanya hivyo. (K.h.j)..

Aina ya majibu yote sio ya kutatanisha isipokuwa kuungama shitaka na kudai kwamba tayari mshitakiwa alikwisha hukumiwa kwa mashitaka hayo hayo husababisha matatizo kadhaa kisheria ambayo tutayajadili baadaye kidogo.

Ikiwa mshitakiwa atakana shitaka basi mahakama yataendelea kusikiliza ushahidi wa upande wa mashitaka ili kuthibitisha shitaka dhidi yake.

Katika kujibu shitaka, kama tulivyogusia juu punde tu, mshitakiwa anaweza kutoa hoja kwamba aliwahi kushitakiwa mahakamani kwa kosa ambalo anakabiliwa nalo sasa na kuwa alitiwa hatiani au aliachiwa huru kabisa.

Ili kuelewa vizuri masharti ya hoja kama hiyo ya mshitakiwa ni vizuri kuona vile ambavyo fungu la 137 la Sheria ya Mwenendo wa Jinai linavyoeleza; ya kwamba:

"Mtu ambaye amewahi kushitakiwa, akapatikana na hatia au kuachiwa huru kabisa na mahakama yenye mamlaka ya kufanya hivyo mintaarafu ya kosa kadha, iwapo uamuzi huo wa mahakama haukubatilishwa au kubadilishwa, mtu huyo hatashitakiwa tena mintaarafu ya kosa hilo hilo na maelezo yale yale".

Hivyo, ili hoja ya mshitakiwa iweze kukubaliwa na mahakama itabidi izingatie na kuthibitisha masharti yafuatayo: Kwanza mshitakiwa awe alipata kushitakiwa kwa aina ya kosa ambalo anashitakiwa nalo tena kwa mara ya pili. Kwa mfano awali alishitakiwa kwa wizi na sasa anashitakiwa tena kwa kosa hilo hilo. Aidha athibitishe kuwa maelezo ya kosa lenyewe ni yale yale.

Kabla hatujaendelea mbele inadhihirika kuwa masharti haya kuhusiana na aina ya kosa linalohusika pamoja na maelezo yake ni finyu sana. Mahakama yamejaribu kuyatafsiri masharti haya kwa upana zaidi kama inavyoonekana katika mashauri haya mawili yafuatayo.

Katika R. v. Absolon Muhanga na Mwenzake (1957 E.A. 660) washitakiwa walikabiliwa na shitaka la kubaka. Wao walitoa hoja kuwa tayari walikwisha shitakiwa na kutiwa hatiani kutokana na kosa la kuvuruga amani na nidhamu katika Jeshi la Polisi, na kwamba maelezo ya shitaka lile la awali na la sasa yalikuwa yale yale.

Hakimu aliyesikiliza shitaka hilo kwa mara ya mwanzo alikubali majibu ya washitakiwa. Jamhuri ilikata rufaa dhidi ya uamuzi huo na mahakama kuu yalisema kwamba ili hoja kama hiyo ikubaliwe, kosa la awali ni lazima liwe sawa na lile la sasa au hata kama sio sawa kabisa basi likaribiane sana. Hivyo ingawa maelezo, na hata ushahidi, mintaarafu ya shitaka la kwanza la kuvuruga amani na lile la kubaka yaliweza kuwa sawa kwa vile yalitokana na tukio moja, bado, kwa kila hali, makosa hayo mawili hayakufanana wala kukaribiana.

Ufafanuzi mzuri zaidi wa sharti hilo ulitolewa katika R. v. Thomas (1949 ALL ER.662) ambapo mshitakiwa alishitakiwa kwamba mnamo Machi, 1949 alimjeruhi mkewe kwa makusudi, akatiwa hatiani. Baadaye mnamo Juni 2, 1949 majeruhi, yaani mke wa mshitakiwa, alifariki. Mshitakiwa alishitakiwa tena kwa kosa la kuua kwa makusudi. Alijibu kuwa alikwisha hukumiwa mintaarafu ya kosa hilo. Yakikataa hoja hiyo ya mshitakiwa, mahakama yalisema:

"Kanuni ya sheria ni kuwa mtu asiadhibiwe mara mbili mintaarafu ya kosa lile lile. Kipimo ni iwapo kosa la awali na lile la sasa yana vipengele sawa vya sheria kwa maana kwamba maelezo ya kosa awali yanatosha kumtia hatiani kwa kosa la pili: sio kwamba maelezo yanayotegemewa na Jamhuri ni sawasawa katika mashauri hayo mawili tofauti". (K.h.j).

Ufafanuzi huo wa mahakama unaondoa mchanganyiko wa fikira kuwa lazima makosa yanayohusika katika mashauri mawili – la kwanza na lile la pili, yawe yanafanana kabisa. Kwa mfano wizi kwa wizi; kubaka kwa kubaka; kuu kwa kuua.

Tafsiri kama hiyo ingekuwa finyu mno na kusababisha utovu badala ya kutenda haki. Lakini sasa ni wazi kuwa muhimu ni iwapo vipengele vinavyofanya makosa hayo kisheria vinafanana kiasi kwamba maelezo yale yale yanatosha kuthibitisha makosa hayo. Hivyo basi kwa mfano mtu anashitakiwa kwa wizi akiwa mtumishi, akaachiwa au kutiwa hatiani, basi madhali uamuzi huo umesimama, hawezi tena baadaye kushitakiwa kwa wizi wa kawaida. Lakini kama awali alishitakiwa kwa wizi wa kawaida akahukumiwa au akaachiwa, anaweza baadaye kushitakiwa tena kwa wizi akiwa mtumishi. Kama awali alishitakiwa kwa mauaji ya kukusudia, akaachiwa huru hawezi tena baadaye akashitakiwa kwa mauaji ya kukusudia. Kwa kawaida iwapo mtu anashitakiwa kwa kosa kubwa ushahidi ukaonyesha kuwa kosa hilo halikuthibitishwa mahakama yanaweza kumtia hatiani kwa kosa dogo iwapo ushahidi utatosha kuthibitisha kosa hilo. (F.300, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Ndiyo maana taarifa nyingi za mauaji ya kukusudia hazijumuishi mauaji ya kutokusudia. Lakini aghalabu hutokea kuwa mahakama humtia mshitakiwa hatiani kwa kosa la mauaji ya kutokusudia baada ya kuridhika na ushahidi ambao awali ulikusudiwa kuthibitisha shitaka la mauaji ya kukusudia.

Sharti jingine muhimu ni kuwa mahakama ambayo awali yalimtia au kumtoa hatiani mashitakiwa lazima yawe yalikuwa na mamlaka ya kusikiliza kosa katika shauri la kwanza. Kwa mfano katika kesi ya R. v. Abloson Mhanga na Mwenzake (I.h.j) mahakama yalielezea kuwa hata kama washitakiwa wangeshitakiwa rasmi kwa kosa la kubaka ka kutiwa hatiani, majibu yao yasingekubaliwa kwa vile mahakama yaliyosikiliza shauri la awali yalikuwa sio mahakama ya sheria bali ni nidhamu za jeshi la polisi. Hivyo basi ikiwa mtu atapatikana na hatia ya kuzinga na maharimu katika mahakama ya wilaya bado baadaye anaweza kushitakiwa tena kwa kosa hilo katika Mahakama Kuu kwa vile mahakama ya awali hayakuwa na mamlaka ya kusikiliza kosa hilo katika shauri lenyewe. Na akiwa ameachiwa huru mintaarafu ya kosa hilo hilo bado pia anaweza kushitakiwa upya katika mahakama kuu, ambayo ndiyo yana uwezo wa kusikiliza mashauri kuhusiana na kosa kama hilo.

Hoja ya mshitakiwa haitakubaliwa iwapo madhara yanayohusika na shitaka la pili yanatokea na kutambuliwa baada ya mshitakiwa kuachiwa huru au kutiwa hatiani kwa kosa la awali katika shauri hilo. Mfano mzuri ni kesi ya R. v. Thomas (I.h.j.) ambayo tumeiona punde tu. Katika shauri hilo mahakama yalisema kwamba ingawa ili kuthibitisha mauaji ya kukusudia ilikuwa ni muhimu kuthibitisha shambulio lililosababisha kifo, kosa lenyewe la mauaji ya kukusudia lilikamilika siku ya kifo cha marehemu na sio pale aliposhambuliwa.

Hoja ambayo tumeizingumzia ina nia ya kuhakikisha kuwa mshitakiwa haadhibiwi mara mbili kwa kosa moja; na kwamba hasumbuliwi mara mbili kwa kosa hilo hilo kutokana na maelezo yale yale. Hoja hii haikubaliwi iwapo mashitaka yaliondolewa dhidi ya mshitakiwa na waendesha mashitaka wenyewe isipokuwa pale ambapo mashtaka yalifutwa kabisa.
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook