Tamko la Makasisi dhidi
ya OIC ni pingamizi la maendeleo
Ndugu Mhariri
TAMKO la Makasisi la hivi karibuni dhidi ya jitihada inayofaywa au hatua inayoweza kuchukuliwa na serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ya kujiunga na OIC ni tamko la kushangaza na ambalo haliwatakii kheri wala maendeleo Watanzania. Si kweli hata kidogo kwamba OIC inavyoelezwa na Makasisi.
Hii ni propaganda yao wanayofanya usiku na mchana kuiweka Tanzania katika ramani ya umaskini, magonjwa, ujinga na madeni ya nchi za magharibi kupitia 'Club' ya Paris. Makasisi huyatumia mazingira haya kufanikisha malengo yao ya kueneza neno na kusimika mizizi yake katika jamii.
Ushahidi upo unaonifanya kusema hivyo na ninapenda kuuweka bayana na wazi. Kanisa katika nchi za Latin Amerika na Cuba lina wafuasi wengi mno, lakini wafuasi hao hao ni maskini wa kupindukia kawaida; na wala halijishughulishi kuwaondolea umaskini wao.
Serikali ya Jamhuri ya Tanzania ina deni kubwa sana ambalo limeanzwa kurejeshwa, lakini ni bahati mbaya deni hilo halipunguki. Halipunguki kwa sababu ya riba. Nchi za Ulaya na Marekani hazitusaidii na kama zina nia ya kutusaidia basi zingetukopesha bila ya riba juu mikopo. Pia inatosha kusema kuwa nchi ya Ulaya na Marekani zimetengeneza dhana ya riba kutunyonya na kujitajirisha kirahisi.
OIC ina tofauti sana na nchi za Ulaya na Marekani. Mfumo wake wa fedha kwa nchi ambayo ni wanachama ni mfumo usiyokuwa na riba. Katika Afrika, OIC imewavutia baadhi ya wengi na sasa wanafaidi na wanajenga uchumi bila machungu makubwa.
Baadhi ya nchi ambazo ni wanachama ni Uganda, Msumbiji, Nigeria, Algeria na kadhalika. Hizi nchi si za Kiislamu, ni nchi kama Tanzania zenye katiba na sera zinazotokana na fikra za watu na wala siyo Qur'an na sira ya Mtume wetu (s). Hivi sasa hakuna anayeweza kuthubutu kuwashawishi waondoke OIC kwani wamefurahia matunda ya uanachama wao.
Hakuna sababu yoyote ya kutishika kuwa Tanzania ikijiunga na OIC itakuwa au italazimishwa kuwa nchi ya Kiislamu. Si kweli hata kidogo kwani Uislamu hauruhusu nguvu katika masuala ya itikadi na imani. Na pia OIC ina katiba na sheria katika uendeshaji wake; wala si Qur'an na sera za Mtume (s). Nuru ya mafanikio ya uchumi katika Afrika ipo katika OIC na shari katika Paris Club.
Leo katika Tanzania tuna wakati wa uwazi na ukweli. Lakini uwazi na ukweli ipewe fursa tu kwa mambo ambayo ni mazuri kwa jamii yetu na siyo kinyume cha hivyo kama wanavyofanya siku hizi baadhi ya watu.
Ninayo sababu ya msingi ya hili. Taasisi ya OIC pamoja na taasisi zilizo chini yake au zilizoundwa na yenyewe, zote zinatambulika na Umoja wa Mataifa kama ni vyombo vya uchumi na fedha, hivyo ni muhimu kwa ustawi wa jamii. OIC ni chombo cha kimataifa na kimekwisha jipatia 'medali' katika kupeleka mbele maendeleo ya jamii mbalimbali.
Makasisi wana mtazamo wao wa mambo ya jamii. Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania isiwafuate Makasisi hao, ila iwaulize Marais Museven wa Uganda, Obasanjo wa Nigeria, Bakiri Muluzi wa Malawi, Chisano wa Msumbiji, wengine wengi na Umoja wa Mataifa.
Hizi ni zama za ukweli na uwazi, hivyo hakuna kuwapa nafasi nzuri Makasisi. Serikali ya Tanzania iwe tayari kuwahurumia wananchi wake ambao sasa wanaishi maisha ya kusikitisha sana, kwa sababu ya madeni yenye riba kutoka nchi za Ulaya na Marekani.
Nilidhani kuwa Makasisi wangeunga mkono Tanzania kujiunga mara moja na OIC lakini dhana haikuweza kuwa kweli. Ukristo wao uko wapi? Wameshindwa kuwa wakweli wa vitabu/kitabu wanavyo/wanachokisimamia. Biblia inakataza kabisa riba. Tabia ya kuishi nje ya Biblia inathibitisha kuwa Makasisi hawamtumikii Mwenyezi Mungu, bali wanatetea maslahi yao.
Haya pia yanapatikana kwa Mayahudi na Maserbia. Inasikitisha sana. Binadamu yuko hasarani kutokana na kufuata fikra na dhana potofu.
Aboubakar S. Marwillo,
P.O. Box 90242,
Dar es Salaam.
Hatutaki Fat'ha za Masheikh
wa CCM
Ndugu Mhariri
NAPENDA kuunga mkono kauli ya Amir wa Waislamu juu ya matusi na kejeli zinazoporoshwa na viongozi wa CCM dhidi ya Waislamu.
Ni kweli kabisa ipo haja ya tabia hii kukomeshwa. Na Masheikh wasioona umuhimu wa kuingia kwenye vita hii wavae kabisa majoho ya kijani utambulisho wao ujulikane wazi na hao tutapambana nao hata fat'ha zao kwenye hafla zetu hatuzitaki.
Shakir Mtambo,
Handeni,
Tanga.
Ndugu Mhariri
NIMEVUTIWA sana na barua iliyoandikwa na Dada Rahma bint Salum yenye kichwa cha habari "ukombozi wa mwanamke ni Uislamu si vinginevyo" iliyopo katika toleo la 207 la Juni 25-31 (Rabiul Awwal 1420). Na hivyo kunipelekea kuandika barua hii.
Tokeo kabla ya kuja kwa Nabii Muhammad (s.a.w.), mwanamke alikuwa anatazamwa kwa namna tofauti, na namna hizo zilionekana wazi kuwa zinamdunisha na kumdhalilisha mwanamke kikomo cha udhalilifu.
Yalipotokea mapinduzi ya viwanda maarufu kama "Industrial Revolution" baada ya vita ya pili ya dunia ndipo msamiati wa "ukombozi wa mwanamke" na "uhuru na usawa" ulipojitokeza ila katika kipindi hicho haukuwa kwa kiasi kikubwa kama hivi sasa.
Kadri miaka inavyozidi kwenda ndipo msamiati huo unapokuwa na harakati zake kupamba moto katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.
Huenda ni kweli, harakati hizi zinataka kumpa mwanamke ukombozi wa kweli, kutoka kwenye yanayoitwa "maonevu" ya mwanamke ambayo yananasibishwa maonevu hayo na Uislamu.
Tatizo ni kwamba, hao wanaoendesha harakati hizo wanafanya kazi wasiyo na elimu nayo, na wanataka kumkomboa mtu wasiyemjua vizuri matokeo yake siku hadi siku, badala ya kumkomboa mwanamke amekuwa akidhalilika na kudunika zaidi, lililo baya zaidi hata yeye mwenyewe haoni kuwa anadhalilika na hivyo kuushangilia "ukombozi" huo aliopewa.
Harakati hizi za ukombozi hivi sasa zimeenea sina katika nchi zetu hizi za Afrika Mashariki na kuna vyama mbalimbali vimewekwa makusudi kuifanya kazi hiyo kama vile TAMWA, TAWLA na vingine vinavyofanana na hivyo.
Katika wakati huu wako wenye maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, mwanamke ndio ameonekana duni zaidi. Hadhi yake imebakia kuwa ni kitu kisichothamani hata iliyokuwa ndogo na hatimaye mwanamke amebakia kuwa kama ni "bidhaa" isiyokuwa na thamani yoyote.
Hivi sasa mwanamke amekuwa ni kivutio cha magazeti ili yanunuliwe kwa kumfanya ni mrembo wa wiki, wapo wanaume wengi hakuna wanalolitafuta kwenye gazeti ila picha za wanawake tu.
Pia amekuwa ni mtu wa kuliingizia shirika la ndege mapato kama mhudumu, ambaye amevishwa kinguo kifupi ili awe kivutio kwa wanaume watakaomtazama.
Mwanamke huyu sasa amekuwa ni kivutio cha biashara, biashara yoyote hata isiyo na uhusiano kabisa na mwanamke pia imemhusisha mwanamke hasa katika matangazo ya biashara. Sabuni mpaka iwe juu ina picha ya mwanamke mzuri, hivyo uzuri aliotunukiwa na Mwenyezi Mungu umekuwa ni balaa kwake.
Pia mwanamke amefanywa ni soko la wahuni, makasino yote yanayojengwa kwa kasi pote ulimwenguni anayefanywa soko humo si mwingine ila ni mwanamke.
Hadhi na heshima yake imeishia kutembezwa uchi juu ya steji kwa kisingizio cha kumtafuta mrembo wa eneo fulani, maarufu kama "Miss World", Miss Lindi, Miss Mtwara" na kadhalika na wanaoandaa vitu vyote hivyo si wanawake wenyewe bali ni wanaume ili kukidhi haja zao na matakwa yao huku akidhalilika mwanamke.
Kinachosikitisha ni kuwa mwanamke mwenyewe hajaona udhalilifu huu na hivyo yeye kuona amependwa na kuthaminiwa kumbe amedhalilishwa na kushushwa thamani yake aliyopewa na Mola wake.
Udhalilifu wote huu hauwezi kwisha mpaka itapofika wakati mwanamke mwenyewe auone udhalilifu huu na kuamua kuchukua hatua za makusudi za kutaka kujikomboa yeye mwenyewe bila kutegemea atakuja mtu mwingine kumkomboa.
Pia mpaka pale atakapoamua kurudi katika Uislamu "Dini ya Maumbile" ambayo mwanadamu ameumbiwa na atoe ukombozi wake tokea humo, kinyume chake itakuwa ni mchezo.
Ukombozi wa kweli wa mwanamke tayari umeshaelezwa ndani ya Qur'an ni jukumu lake mwanamke kuutafuta yeye mwenyewe hata siku moja mtu huwa hakombolewi mpaka pale atakapoamua kujikomboa mwenyewe katika maeneo ambayo wanaharakati hao wanadai mwanamke amenyimwa haki zake na Uislamu ni katika mavazi, ndoa hasa ile ya mke zaidi ya mmoja, mirathi na kadhalika.
Wakati kote huko kumeshabainishwa wazi na Qur'an na anayetaka ufafanuzi zaidi arejee Qur'an (4:19), (24:30-31), 33:59), (2:222), (4:8), (4:12-13) na kadhalika.
Wakati umefika sasa kwa wanawake kutambua na kutanabahi juu ya ukweli kuhusu ukombozi wao, kinyume chake watazidi kuwa dhalili kwani sasa njia ya kuwadhalilisha ziko wazi wala hazihitaji nguvu kuzitafuta. Na kama watauona ukweli huu basi maangamizi yao yataendelea kila siku kwani mwanamke amegeuzwa chombo cha starehe na kurahishia starehe hizo akarahisishiwa njia za kutoa mimba jambo ambalo ni maangamizi kwa maisha ya mwanamke.
Fatma bint Mussa,
Mtwara.
Sasa kumekucha
Ndugu Mhariri
NAOMBA unipe fursa kidogo niseme kuwa sasa kumekucha. Wenye tongotongo zao machoni wanawe au wakajifiche.
Kauli ya Amir wa Shura ya Waislamu Dar imetupa faraja na changamoto ya kupambana na madhalimu.
Natoa wito kwa Waislamu wote popote walipo katika Misikiti yao na jumuiya zao, kazi ni moja tu; kibano kwa CCM. Rafiki mfanye rafiki adui mfanye adui.
Yusuf Mollel,
Arusha.
Komeni kuwatukana Waislamu
Ndugu Mhariri
KAULI za baadhi ya viongozi wa CCM na serikali yake katika majukwaa ya kisiasa ni za kusikitisha sana.
Hawaoni raha ila wawakejeli Waislamu. Mara hawana elimu, mara wanahongwa vibandiko, mara siasa kali na mengine kama hayo.
Pengine dhana yao huo ni mchezo wa kuigiza, lakini hicho ndicho kitanzi chao. Na Wachechen washawapelekea salamu juzi. Sasa na waendelee tu waongeze joto kwenye maji ikifika 100 0C wamekwenda.
Bi. Faidha S. Salim,
Dar es Salaam.
Masheikh tupeni msimamo
Ndugu Mhariri
WIKI iliyopita Amir Mkuu wa Waislamu Dar es Salaam alituarifu kwamba fikra inafanywa ili kukomesha tabia ya viongozi wa CCM na serikali yake kuwakejeli na kuwatukana Waislamu.
Nawaomba Masheikh wetu wa Mwanza watuelekeze sisi tufanye nini dhidi ya watu hawa wanaotutukana kila leo au tungoje maelekezo toka Dar.
Zuberi Saidi,
Mwanza.
Ndugu Mhariri
NAPENDA kuchukua fursa hii katika gazeti hili takatifu ili niweze kuwapongeza Maimamu wote wa Dar es Salaam kwa ushiriakiano wao na juhudi zao za pamoja ambazo zimefanikisha kumchagua Amir wa Dar es Salaam Sheikh Juma Mbukuzi kwa kufanya hivi ni hatua muhimu sana ambayo iliyokuwa inasubiriwa na Waislamu kwa muda mrefu.
Kwa hiyo sisi Waislamu tunaahidi kuwa bega kwa bega na Amiri wetu wakati wowote na sehemu yoyote na hi isiishie hapa tu Dar es Salaam bali mpango huu unatakiwa uenee mpaka mikoani na mwishowe achaguliwe Amir Mkuu wa Tanzania nzima kwa sababu sisi Waislamu tunataka viongozi shupavu kama alivyokuwa Mtume wetu Muhammad (s.a.w.) na maswahaba zake hatutaki viongozi wa kanzu na vilemba wala viongozi wa kwenda kuhiji kila mwaka bila ya kujali wanaowaongoza wanahitaji nini..
Khamis Khamis
Al-Furqan Islamic Sec.
School,
Dar es Salaam.
|
|