UJUMBE WA IJUMAA
 
Ujumbe huu!
 

Na Tahir Rashid

NI WATU! Ndio tusiojua kuwa mfundishaji ni Allah (12:68). Wengi wetu hatujui jambo hili. Elimu! Allah ametufundisha kwa wasita wa kalamu (96:4). Tambua haraka; Kalamu hii ni kalamu ya Kimungu. Na wala sio kalamu zetu na vitabu vilivyoandikwa na watu! Watu wamechukua vitabu vya Allah-Taurati ... Qur'an ambavyo ni Nuru na Uongozi kwa watu, na kuvichanganua kwa kuandika vitabu vyenye juzuu kemkem (6:91) za yale tunayoyataka ili kupoteza umma wa ulimwengu uitwao ulimwengu wa tatu.

Mwalimu wetu Allah katufundisha nini?

Katufundisha kunena (55:4) kwa sababu ametuumba kwa kiasi (55:49) na amri yake ni mara moja (55:50). Na ingawa hatukumbuki, wenzetu waliotangulia walishaangamizwa (kwa kutoyazingatia mafunzo yake) (55:51). Kwani kila jambo dogo na kubwa huandikwa daftarini (55:52-53). Vyombo vya kufanyia mitihani, navyo ni macho na masikio (72:2). Kisha tutaulizwa juu ya neema (tulizopewa tulizitumiaje) (102:8).

Allah kwa kufutanyia wepesi, kwa sababu mwanadamu ni dhaifu (4:28), ametufundisha mambo ambayo tulikuwa hatuyajui (96:5) (55:2) (ndipo) akatuumba (55:3).

Yu anaapa Allah kwa kila kilichozaa kila kilichozaliwa kuwa tumeumbwa kutaabika, huku hudhani hakuna yeyote atakayetuweza! (90:3-4). La! Anaapa tena Muumba wetu kuwa hakuna nafsi yoyote ila inayo mchungaji juu yake (86:4).

Ewe mtu!

Ni nini kikudanganyacho na Mola wako mtukufu (hata ukamwasi) (82:6). Aliyekuumba na kukutengeneza, kisha akakulinganisha sawa. Katika sura yeyote aliyoipenda amekutengeneza (82:7-8). Na hakika juu yetu kuna wenye kutufunza watukufu wenye kuandika. Wanajua yote tunayoyatenda (82:10-12). Kwani matendo yetu si mengine bali ni kukadhibisha dini (utaratibu wetu wa maisha aliyotupangia kiongozi wetu, Muumba wetu Allah) (82:9). Viumbe wenzetu mwendo wao waenda sawa isipokuwa mwanadamu. Hakika sisi ni madhalimu na wajinga (33:72).

Dini:

Kinachotakikana hapa sio dini tu, eti ili kila mtu apate nafasi ya kutia lake. Hapana! Dini ya Mwenyezi Mungu (110:2) kama tunavyosoma kwenye suratil Nasr aya ya pili:

"Na ukiwaona watu wakiingia katika Dini ya Allah makundi makundi... (110:2) hiyo ndiyo dini tunayoitaka tujue na kuifuata.

Na dini mbele ya Allah ni kuwa Muungwana (3:19) kama anavyotuthibishia Muumba wetu: "Na tukambainishia zote njia mbili (ilio mbaya na iliyo nzuri) (190:10). "Je! Amekukata huo mlima (kizuizi kimkingacho na njia njema)?" (90:11).

"Na nini kitakachojulisha huo mlima (kizuizi kinachokukinga na hiyo njia njema usione?" (90:12). "(Kukiondoa kizuizi hicho kikukingacho) ni kujitoa utumwani na kuwa muungwana (90:13). "Kisha uwe miongoni mwa walioamini na kuhusiana kusubiri na kuhusiana kuhurumiana". (90:17). "Hao ndio watu wa upande wa kheri". (90:18).

Watu wa kheri:

Ni tamaa ya kila mwanadamu kuishi milele na kwa raha nyingi na matumizi ya kila namna. Lakini mwanadamu yuko katika taabu na kufanya yatakayomdhuru. Mola wetu anatuitia kwenye kheri, lakini tunamkimbia. Wallahi tuko katika upotofu ulio dhahiri, tunapowafanya sawa na Mola wa walimwengu wote, wale watu wabaya (tuliowapigia kura) (26:97-99); nao ndio wakuu wetu wa nchi (6:123). Kiongozi wetu khaswa ni Allah (2:120). Tukimpa kura zetu na kumuitikia tutapata wema (13:18). Kuishi milele katika vivuli vya mikunazi isiyo na miiba, na migomba iliyopangaliwa mazao yake, mabomba yametuzunguka kila upande yenye mmiminiko mzuri. Na matunda mengi msimu wake ni wenye kuendelea, wala hayana mwenyewe hivyo hayakatazwi. Na kila watu wanachokipenda - wanawake watukufu wenye umbo zuri, miguu ya ndovu, umri wao miaka 18-21. Wawe wanapendana na waume zao ambao ni rika moja. Niambie ni Kigogo yupi tumpe kura zetu mwenye uwezo wa kutupa haya?

Hawa tunaowapa uongozi (28:41) wasiojua lolote (10:89) na kuwapenda (2:165), wamepotea kwa sababu hufuata matamanio yao pasi na uwongozi utokao kwa Allah (28:50) (wao hudai kuwa uongozi wao hauna dini). Kwa hiyo siku tutakapoitwa na kuulizwa "wako wapi washirika wangu (ambao uongozi wao mliuthamini zaidi yangu) ambao mlikuwa mkidai (kuwa ni viongozi wazuri) (28:61) tena kwa ajili yao mkigombana (16:27)? Siku hiyo tutadhalilika kabisa (37:26). Hapo ndipo mashahidi watakapoletwa tuambiwe "leteni hoja zenu". Yale tuliyoyazua (kuabudu vyeo tulivyopanga sisi wenyewe 12:40) yatatupotea (28:75). Na hata kama tutawaita washirika wetu (waliokuwa na madigrii, Mapadri na Masheikh 9:31) hawatatujibu (28:64). Bali tutabaki kulalama: Wanyonge kuwalilia wakubwa; "Kama si nyinyi bila shaka tungekuwa waumini (34:31)". Viongozi wetu (wanavyuoni na watawa 9:31 ambao wametuundia (tasjili) dini kemkem ambazo Allah hakuzitolea kibali 42:21). Watatujibu waseme: Oh! Sisi tulikuzuieni uongozi (wa Allah) baada ya kukufikieni? (Siyo) bali nyinyi wenyewe mlikuwa maasi (34:32) kwa kukanusha kwenu kupwekeka kwa Allah (37:34-35). Hivyo (mkatupigia kura) mkatujaalia kuwa miungu (viongozi) pamoja na Allah (15:95-96)". Ndipo watakaponadi:

"Mola wetu! Hawa ndio tuliowapoteza kama tulivyopotea; tunajiepusha nao mbele yako. Hawakuwa wakituabudu sisi (28:63) wala hatukuwa na habari ya ibada yao (10:28-29)". "Hatukuwa na mamlaka juu yenu, bali nyinyi wenyewe mlikuwa wapotofu (37:30), mlikufuru na kuzidi (3:90)".

Ndipo Malaika waulizwe: Je! Hawa walikuwa wakiwaabudu? Waseme: "Umeepukana na kila upungufu! Wewe ndiwe kipenzi chetu, sio hao, bali walikuwa wakiwaabudu majini (34:40-41)".

Majini:

Wakuu wa miji ndio waovu (6:123) Ikawa humo wanafanya hila na vitimbi (katika vikao vya chama vya siri na dhahiri, na katika vikao vya bunge) usiku na mchana, (hivyo) wakaamuru watu (mashambani) kumkufuru Allah na kumfanyia washirika (kuchagua viongozi) (34:33). Hivyo watu wakamfanyia Allah majini kuwa washirika wake (kwa viongozi pamoja naye) hali Yeye ndiye aliyewaumba (16:100). Na ajabu katika kampeni ya Allah na majini, majini yamechukua wafuasi wengi katika watu! (6:128).

Je! Tujiulize hawa majini wanaofuatwa na watu (98 kwa mia ya Watanzania huishi mashambani) ni nani hao? Kama si vile lugha imepindwa, jawabu lingekuwa rahisi.

Fahamu kwamba watu wanaoishi mashambani kilugha huitwa Washamba. Na watu wanaoishi kama vile Uchina huitwa Machina. Lakini ukija kuuliza je! Watu wanaoishi mijini huitwaje? Watakujibu "wanamji". Ah! Kama wanaokaa Uchina huitwa Machina, basi wale wanaoishi mijini hao ndio kwa lugha fasaha huitwa Majini. Mtu anayekaa shamba ni mshamba huyo. Mtu anayekaa mjini ni jini hilo. Mtu anayekaaa kijijini ni kajini (kadogo) kwani wao wa vijijini mila wamezitupa na kufuata matamanio yao (45:23) (Iblisi) na Iblisi ni miongoni mwa majini.

Ndio mababu zetu wema (weusi) miaka isiyofika mia mbili iliyopita walikuwa na (kibla) mahala pa kuchinjia mihanga ya ibada ili kulitaja jina la Allah juu ya vile alivyowazuruku katika wanyama hao wenye miguu minne (maisha ya bustanini 22:34) Maisha ya kuhama hama na mifugo yao. Wakiishi maisha ya kidugu (kumbuka waumini ni ndugu) ili walazimishwe kuishi mashambani walime mazao ya kulisha viwanda Ulaya, wakalazimishwa kulipa kodi. Na hapa wakaanza kuvunja maisha ya udugu ambayo mali ilikuwa ya jamii nzima. Na hapa sasa watu wenye nguvu wakaanza kumiliki ardhi na mifugo. Na wale waliokosa wakaanza kufanywa watumwa na wenye nacho.

Mashambani sasa vijiji viakota na kushurutushwa wanavijiji kuwa na viongozi ambao hushughulikia dunia. Mihanga ya ibada zao huchinjwa kwa ajili ya viongozi wao na wakuu wanaotaka mijini. Na marafiki zao (wakuu wa miji) katika watu wa mashambani na vijijini hunufaishana (6:128). Viongozi wa vijijini na mashambani hukusanya kila aina ya kodi kuwapelekea wale wakuu wa wilaya, mikoa na taifa. Nao hupata mishahara na asilimia fulani katika yale waliyoyakusanya.

Wakuu hawa wanapoambiwa "msifanye uharibifu nchini" husema: "Sisi tunajenga nchi" (2:11) nao hawatambui kuwa wanaharibu (2:12). Nakumbuka nikiwa na miaka kumi (1960) majirani tulikuwa tunapeana nyama kila leo. Lakini baada ya kuwa na kiongozi anayeitwa Rais maduka ya kuuza nyama yakazuka. Wakati huo kilo moja ilikuwa shilingi moja na nusu. Na kila mtu aliweza kununua... Lakini leo kilo ya nyama ni shilingi elfu moja. Ni watu wa mijini (majini) ndio wenye mbavu za kula nyama na starehe ya nyama choma. Je! Watu mashambani waliotegemea mchicha na chumvi aliouotesha Allah bure! Na sasa mvua zimegoma hata maji ni ya kununua - maneno yake Allah, hayajawa kweli?

"Wakuu wetu wa miji ni maadui (6:112) wametutoa bustanini na kutubwaga mashambani, vijijini na leo mijini, sasa tuna njaa, tuko uchi tuna kiu na joto (global heating) ni balaa (20:117-119) huku wanatushadidia maisha marefu na maisha ya raha (maisha ya kifalme) (kuwa na nyumba nzuri, vipando, barabara safi na kula vizuri ) (20:120) kumbe wanatucheza shere (2:14). Wanapokuwa peke yao kwa mashetani wao huwaambia: "Hakika sisi tuko pamoja nanyi" (2:14).
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook