Na Mwandishi Wetu
AMIR wa Shura ya Maimamu Sheikh Juma Salim Mbukuzi amesema amani ya nchi itadumu kwa serikali kutenda haki bila upendeleo huku ikishughulikia madai ya wananchi badala ya kukaa kimya au kutumia vitisho na mabavu.
Aliyasema hayo jana wakati akizungumza na watu mbali mbali waliomtembelea nyumbani kwake Mburahati Barafu jijini.
Alisisitiza kuwa madai ya Waislamu ni haki kwa mujibu wa Katiba ya nchi na tamko la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa.
Sheikh Mbukuzi aliachiwa kwa dhamana juzi baada ya kukaa rumande kwa takriban wiki tatu akidaiwa kutoa maneno ya uchochezi kwa mujibu wa sheria ya magazeti.
Alikamatwa Septemba 17 kufuatia mazungumzo yake na waandishi wa habari Jumatano Septemba 15 katika Msikiti wa Mkwajuni Kinondoni, Jijini.
Awali alifikishwa mahakamani mchana wa Septemba 17 ambapo baada ya kusomewa shitaka la kutishia kumwaga damu aliwekwa rumande hadi Septemba 20.
Alipofikishwa tena mahakamani tarehe hiyo (Septemba 20), Mwendesha Mashitaka wa Mahakama ya Kisutu mrakibu wa polisi Bwana Leonard Mashaka alidai mbele ya Hakimu anayesikiliza kesi hiyo Mama Eliaman Mbise kuwa Sheikh huyo alikuwa akituhumiwa kutoa maneno ya uchochezi ambayo ni kinyume na kifungu Na. 3 cha Sheria ya Magazeti ya 1976.
Maneno hayo kwa mujibu wa nakala ya mashitaka ni pamoja na kuhadharisha kuwa utendaji wa serikali unaweza kuwapelekea Waislamu kujihisi wao ni makabwela wasiothaminiwa katika nchi yao hali ambayo huenda ikaitumbukiza nchi katika umwagaji wa damu iwapo wanaodhulumiwa watashindwa kuvumilia.
Baada ya kusoma shitaka hilo Mwendesha Mashitaka alimuomba Hakimu azuie dhamana kwa mtuhumiwa kwa kuwa 'kosa' alilotenda ni zito linaloweza kutishia amani nchini na amefanya hivyo akiwa katika dhamana ya kesi nyingine inayomkabili.
Hata hivyo mawakili wanaomtetea wameeleza kuwa madai aliyoyatoa mwendesha mashitaka hayakuwa na msingi kwa sababu dhamana ni haki ya kikatiba ya mshitakiwa na kwamba tangu hapo mahakama bado haijathibitisha kisheria kosa hilo hivyo kumnyima mtuhumiwa dhamana ni sawa na kumuhukumu kuwa ni mkosa kabla ya shauri halijasikilizwa.
Sheikh Mbukuzi alifikishwa tena mahakamani Jumatatu wiki hii hata hivyo ilidaiwa kuwa Hakimu anayesikiliza kesi hiyo mama Mbise hakuwepo badala yake Hakimu mwingine Bwana Ezekiel Ligema aliiahirisha hadi Oktoba 18 mwaka huu.
Siku ya jumatano wiki hii ghafla alifikishwa tena mahakamani ambapo Hakimu wa kesi hiyo Mama Eliaman Mbise aliamuru dhamana iwe wazi kwa masharti kwamba asijihusishe na 'vikundi' vya uchochezi.
Akijibu swali la mwandishi kuhusu masharti ya mahakama na wajibu wake kama Amir na Imamu wa msikiti, Sheikh Mbukuzi amesema msikiti ni jengo la ibada na Waislamu ni sehemu ya Wananchi wa nchi hii hivyo ataendelea kuikumbusha serikali akiwa kama kiongozi wa jamii hapa nchini kama wafanyavyo viongozi wa dini nyingine..
Alisema kwa kutekeleza wajibu huo ndiko kutaiepusha nchi na migogoro inayoweza kuipelekea katika maangamizi.
Alirudia kusisitiza wito wa Waislamu wa kuitaka serikali iunde Tume Huru kuchunguza suala la Mwembechai ambalo polisi iliripotiwa kuvamia Msikiti, kupiga na hatimaye kuua Waislamu mwezi Februari mwaka jana.
Wakati huo huo, Sheikh Juma Mbukuzi anatazamiwa kuzungumza na Waislamu leo baada ya swala ya Ijumaa katika Msikiti wa Tungi ulioko Temeke jijini.
Sheikh Mbukuzi ambaye pia
ni Amir wa Waislamu jijini ameahidi kuzungumzia mambo mbalimbali yanayowahusu
Waislamu ikiwa ni pamoja na nafasi yao kama wananchi wa Tanzania.
--
|
|