IJUE SHERIA
 
Kukata rufaa

Dk. Abdallah J. Saffar
 

UKIACHILIA mbali pale ambapo adhabu ndogo imetolewa (F.360(2), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, Na. 1 1985. Hata hivyo, kwa ruhusa ya Mahakama Kuu, rufani inaweza kukatwa kupinga uhalali na uzito wa adhabu) au pale ambapo mshitakiwa amekiri kosa na kutiwa hatiani (F.360(1), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, Na. 2, 1984), rufaa inaweza kukatwa dhidi ya uamuzi au hukumu yoyote ile ya mahakama ya awali.

Ndiyo kusema rufaa huweza kukatwa kutoka Mahakama Kuu ya Mwanzo kwenda Mahakama ya Wilaya (F.20(1), Sheria ya Mahakama ya Mahakimu, Na. 2, 1984) au Mahakama ya Hakimu Mkazi, kutoka hapo kwenda Mahakama Kuu (F.359(1), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j) na kama lazima hadi Mahakama ya Rufani ya Tanzania (F.3(1), Sheria ya Mamlaka ya Rufani, Na. 15 1979).

Katika kusikiliza rufaa mahakama yanayohusika yanaweza kubatilisha uamuzi au hukumu ya mahakama ya awali na kumwachia huru mrufani au yanaweza kuamuru shauri lisikilizwe upya na hakimu yule yule au mwingine (F.366(1)(a)(i), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Aidha, mahakama yanaweza kubadilisha, kuipunguza au kuiongeza adhabu iliyotolewa mwanzo (K.h.j). Kwa jumla yanaweza kupitisha amri nyingine yoyote muafaka kadiri inavyostahiki kulingana na mazingira ya shauri lenyewe (K.h.j).

Namna ya kukata rufaa

Ni wajibu wa mahakama kumwelewesha mshitakiwa haki yake ya kukata rufaa mara baada ya kumtia hatiani (K.h.j). Muhimu vile vile ni kuzingatia ukomo wa muda uliowekwa kutoa taarifa ya kukata rufaa na kuwasilisha hati ya kukata rufaa yenyewe mahakamani.

Taarifa ya kukata rufaa na hati ya kukata rufaa ni mambo mawili muhimu sana ingawa ni tofauti kwa kila hali. Ya kwanza ni ile taarifa tu kuyaeleza mahakama yanayohusika haja ya kufanya hivyo, ambayo ni budi itolewe katika muda usiozidi siku kumi kutoka Mahakama ya Wilaya kwenda Mahakama Kuu (F.361, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j), na siku kumi na nne kutoka hapo kwenda Mahakama ya Rufani Tanzania (K.61, Kanuni za Mahakama ya Rufani, Tangazo la Serikali Na. 102 la 28 la 28 Septemba 1979). Ni kwa sababu za maana tu maombi ya kutoa taarifa ya kukata nje ya wakati uliowekwa yanaweza kukubaliwa ( F.361, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j).

Hati ya kukata rufaa ni karatasi rasmi yenye hoja za kupinga amri, uamuzi au hukumu ya mahakama ya awali. Hii ni lazima iwasilishwe mahakamani katika muda wa siku thelathini iwapo ni Mahakama ya Mwanzo kwenda Mahakama ya Wilaya (F.20(3), Sheria ya Mahakama ya Mahakimu, i.h,j) siku arobaini na tano kutoka hapo kwenda Mahakama Kuu (F.36(b), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j), na siku kumi na nne tu kwenda Mahakama ya Rufani Tanzania (K. 65, Kanuni za Mahakama ya Rufani Tanzania, i.h.j). Siku zinaanza kuhesabiwa pale mrufani anapoupata mwenendo wa shauri ambalo kwalo anakusudia kukata rufaa. Na kama vile katika taarifa ya kukata rufaa, muda wa kuwasilisha hati ya kukata rufani unaweza kuongezwa tu kutokana na sababu za msingi.

Taarifa ya kukata rufaa inahitajika kuandikwa kwa undani au utaalamu kama ilivyo hati ya kukata rufaa. La muhimu zaidi ni kuonyesha mahakama yanayohusika, namba ya shauri, wa wale wahusika wenyewe, halafu, kwa muhtasari, kueleza ni nia wala sio sababu, ya kukata rufaa. Kwa mfano taarifa hiyo inaweza kuandikwa jinsi ifuatavyo:

Mahakama ya Wilaya ya Mbozi Vwawa, Shauri la Jinai Na. 15 la 1994 Kutoka Mahakama ya Mwanzo Mpiji kati ya Kinenge Mkakati Mrufani na Jamhuri Mrufaniwa.

TAARIFA YA KUKATA RUFAA

Hii ni taarifa ya kukata rufaa kwenda Mahakama ya Wilaya dhidi ya hukumu iliyotolewa na Hakimu Gabriel Mtarimbo Juni 8, 1994 katika mahakama yaliyotajwa hapo juu ambapo nilionekana na hatia ya kosa la wizi na kuadhibiwa kifungo cha miezi tisa.

Sahihi,

Kinenge Mkakati

Januari 5, 1995, Vwawa. Nakala kwa: Wakili wa Serikali.

Isipokuwa kwa taarifa ya kukata rufaa kwenda Mahakama ya Rufani ya Tanzania tu (K.h.j) taarifa za kukata rufaa kutoka Mahakama nyingine zozote zile hazitakiwi, kisheria, kuwa na sura mahsusi. La maana ni kutoa maelezo ya lazima kumfanya karani wa masjala ya mahakama ambayo rufaa inakusudiwa kukatwa kuweza kutekeleza wajibu wake.

Baada ya taarifa ya kukata rufaa kuwasilishwa mahakamani mrufani atapelekewa nakala ya mwenendo wa shauri linalohusika ili atayarishe rasmi hati ya kukata rufaa. Iwapo kwa sababu ya maana mathalan, mrufani anashindwa na kuchelewa kutayarisha au kuwasilisha mahakamani hati ya kukata rufaa katika muda uliowekwa na sheria, itabidi aandike maombi ya kukata rufaa nje ya muda unaotakiwa (F.361(b), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Maombi hayo itabidi yaambatane na kiapo cha maandishi kuelezea sababu zilizomzuia kushughulikia rufani katika wakati unaotakiwa. Kiapo ni lazima kipatiwe ushuhuda wa mwapishaji kama vile wakili, hakimu au mlinzi wa amani.

Ukomo wa muda wa kutoa taarifa ya kukata rufaa pamoja na kuwasilisha hati ya kukata rufaa umewekwa kwa sababu maalum. Mosi kuyataarifu mahakama kwamba shauri linalohusika bado linaendelezwa katika hatua ya juu hivyo vielelezo vyote vilivyohusika awali, iwapo vipo, visirejeshwe kwa wenyewe taraa vitahitajika tena wakati wa kusikiliza rufani yenyewe (R.v. Anastasia Menge, 1974 L.R.T. n.46).

Kwa kawaida muda wa kutoa taarifa ya kukata rufaa ukipita, mahakama ya awali huvirejesha kwa wenyewe vielelezo vilivyohusika au kuvishughulikia kwa jinsi nyingine yoyote ipasavyo, na wala sio kabla ya hapo (K.h.j).

Pili, kumpa taarifa mrufaniwa, aelewe kwamba mambo hayajamalizika hivyo awe tayari kujiandaa kwa hoja za kuiunga mkono hukumu iliyotolewa awali kumpa haki. Ni kanuni maridhawa ya utoaji haki kuwa kila mhusika awe na muda wa kutosha kujiandaa na utayarishaji wa uendeshaji mashtaka au utetezi wake.

Tatu, haki budi itolewe mapema ipasavyo. Sio busara miezi kadhaa baada ya hukumu ya awali, au yoyote ile nyingine kutolewa, mtu aruhusiwe kukata rufani kubatilisha amri, uamuzi au hukumu ya awali.

--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook