Moyo wa Upendo wa TANU ndio utakaodumisha Umoja
 

MWALIMU alianza siasa za kudai uhuru wa Tanganyika katika mazingira ya Dar es Salaam akiwa amezungukwa na Uislamu na Waislamu. Kulikuwa na tofauti kubwa kati ya kiongozi huyu na wale aliowaongoza. Siku hizo Mwalimu kijana mdogo wa miaka thelathini. Kivazi chake kilikuwa ni kaptula na soksi za stokingi. Mavazi rasmi ya wasomi wa miaka ya thelathini.

Katika TAA aliwakuta vijana wenzake. Marehemu Abdulwahid Sykes na mdogo wake Ally, Waziri Dossa Aziz na wengineo. Halikadhalika walikuwepo vijana wengine kama Hamza Kibwana Mwapachu, Steven Mhando na Zuberi Mtemvu. TANU ilipoundwa mwaka 1954 kukawa na baraza la wazee chini ya Sheikh Suileman Takadir. Baraza hili lilijumuisha wazee wengi maarufu wa mjini na Masheikh. Katika hali kama hii ungelidhani kuwa Mwalimu angejihisi yupo ugenini. La hasha, Mwalimu alikaa vyema katika kundi la Waswahili na Masheikh.

Mwalimu siku moja katika kuwakumbuka rafiki zake wa zamani akizungumza na Dossa Aziz na wageni wengine nyumbani kwake Msasani, katika kuelezea kile alichokiita "the TANU spirit" yaani moyo wa upendo wa wana-TANU, alisema kuwa, siku moja wakati wa kudai uhuru alikuwa anatoka nyumbani kwake Magomeni akija Kariakoo kwa miguu kuelekea sokoni kutafuta mahitaji yake, lakini mfukoni alikuwa hana senti moja. Njiani akakutana na Mzee Mshume Kiyate. Alipomuuliza anakwenda wapi, alimfahamisha kuwa anakwenda sokoni lakini hana fedha za kununua chochote. Mzee Mshume aliingiza mkono katika koti lake na akatoa shilingi mia mbili akampa. (Ukitaka kujua thamani ya fedha hizo ikutoshe tu kuwa nyumba ya vyumba sita kujenga Kariakoo ilikuwa inagharimu shilingi mia tano). Kutokana na hali hii Mshume Kiyate aliona itakuwa ni kumtwisha Mwalimu mzigo mzito ikiwa atakuwa anashughulika na kuwatafutia wanawe chakula na wakati huo huo anafanya kazi za TANU. Mzee Mshume akajitolea kuihudumia nyumba ya Mwalimu kwa chakula. Alifanya hivyo hadi uhuru ulipopatikana.

Baada ya uhuru Mwalimu alimwomba Mzee Mshume aache kufanya hivyo lakini alikataa na akamtafadhalisha Mwalimu aendelee kula chakula chake na kile ambacho kinatolewa na serikali kwake yeye kama mkuu wa nchi alimuomba Mwalimu awape wageni wake. Baada ya maasi ya wanajeshi wa KAR tarehe 20 Januari, 1964 kuzimwa na jeshi la Kiingereza, TANU ilifanya mkutano mkubwa sana Jangwani. Mzee Mshume kwa niaba ya wazee wa TANU alipanda jukwaani na kumvisha Mwalimu kilemba kama ishara ya kuunga mkono uongozi wake.

Pengine ni vyema tuangalie mtiririko wa kupigania uhuru wa nchi hii ili tuone mchango wa Mwalimu na tupate kumuenzi:

1929: TAA yaundwa ikiwa na wajumbe wafuatao:

1. Kleist Sykes, 2. Mzee bin Sudi, 3. Ibrahim Hamis, 4. Zibe Kidasi, 5. Ali Said Mpima, 6. Suleiman Majisu, 7. Raikes Kusi, 8. Rawson Watts, 9. Cecil Matola.

1950: TAA yawasiliana na KAU; Abdulwahid alikwenda Nairobi kukutana na Jomo Kenyatta ili kujenga mawasiliano na chama cha Kenya African Union (KAU).

1951: Kuundwa kwa tawi la siasa la TAA; likiwa na wajumbe wafuatao:

1. Abdulwahid Sykes (Secretary)
2. Sheikh Hassan bin Amir
3. Hamza Kibwana Mwapachu.
4. Said Chaurembo
5. Dk. Kyaruzi.
6. John Rupia.
7. Stephen Mhando

1951: Kenyatta akutana tena na viongozi wa TAA. Safari hii mkutano huo ulifanyika Arusha. Wajumbe wa TAA walikuwa Abdulwahid Kleist Sykes, Dossa Aziz na Stephen Mhando.

1952: Abdulwahid alichaguliwa kuwa Rais wa TAA.

1952: Mwalimu Nyerere atambulishwa kwa Abdulwahid na Bwana Kasela Bantu. Baada ya utambulisho huo ikawa kila Jumamosi Mwalimu Nyerere akawa anakutana na akina Dossa Azizi, Bw. Ally Sykes, Abdulwahid Sykes, Dustan Omar na Mhando kujadili mustakbali wa nchi ya Tanganyika.

Mikutano hiyo ama ilikuwa ikifanyika nyumbani kwa Dossa Azizi mtaa wa Congo au mtaa wa Stanley nyumbani kwa Abdulwahid.

Alikuwa ni Dossa Azizi ambaye mara nyingi alikuwa akimrudisha Mwalimu Nyerere kwa gari lake Pugu (St. Francis College) baada ya mkutano.

1953: Mwalimu achaguliwa kuwa Rais wa TAA. Wazee waliompa nguvu ya kisiasa Mwalimu mara baada ya kuingia katika TAA/TANU.

Sheikh Hassan bin Amir, Sheikh Suleiman Takadir, Mzee Mohammed Jumbe Tambaza, Mshume Kiyate na Mwinjuma Mwinyikambi. Wengine walikuwa Rajab Diwani, Makisi Mbwana, Sheikh Haidar Mwinyimvua na Idd Faiz Mafongo. Aidha walikuwepo Idd Tosiri, Sheikh Mohamed Ramia na Mashado Ramadhani Plantan.

Oktoba 10, 1953 Mwalimu Nyerere, Abdulwahid Sykes, Ally Sykes, Dossa Aziz na John Rupia walikutana kujadili namna ya kuibadili TAA kuwa chama kamili cha siasa.

1954: TANU yaanzishwa. Wajumbe wa mkutano uliojadili kuibadili katiba ya TAA kuwa TANU walikuwa Abdulwahid Sykes, Julius Nyerere, Tewa Said Tewa, Dossa Aziz, Ally Sykes, Kasela Bantu, , Abubakar Ilanga na Saadan Abdu Kandoro. Wengine walikuwa S.M. Kitwana, C.O. Milinga, Patrick Kunambi, Gerimano Pacha, Japhet Kirilo na L.M. Makaranga. Walikuwa pia Joseph Kimalando na John Rupia.

Mkutano wa kuizindua rasmi TANU ulihudhuriwa na wajumbe wafuatao: Julius Nyerere, Abdulwahid Sykes, Ally Sykes, Dossa Aziz, John Rupia na Mshume Kiyate. Wengine walikuwa Makisi Mbwana, Jumbe Tambaza, Juma Waziri, Clement Mtamila, Rajab Diwani, Schneider Plantan na Marsha Bilali. Walikuwepo pia Rashid Ally Meli, Frederick Njiliwa, Idd Faiz Mafongo, Idd Tulio, Denis Phombeah na wengine.

Julius Nyerere alipewa kadi ya TANU Na. 1, kadi Na. 2 ikaenda kwa Ally Sykes na Abdulwahid akachukua kadi ya TANU Na. 3, Dossa Azizi alichukua kadi Na. 4, kadi Na. 5 ikaenda kwa Phombeah. Dome Okochi alipata kadi Na. 6, John Rupia Na. 7, Bibi Titi Mohamed kadi Na. 16 na Idd Tosiri kadi Na. 25.

Itaendelea toleo lijalo.
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook