Wanaodaiwa vibaraka wasuswa mkutanoni
 

MAIMAMU jijini Dar es Salaam walimelikana Baraza la Maimamu ambalo wiki hii liliitisha kikao cha Maimamu kujadili suala la Kadhi.

Maimamu hao waliwaambia viongozi wa Baraza hilo kuwa wao hawako pamoja na Baraza hilo na kwamba wanaitambua Shura ya Maimamu inayoongozwa na Sheikh Juma Mbukuzi kuwa ndiyo chombo kinachowaunganisha.

Wakizungumza katika mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Starlight jijini Jumatatu wiki hii, Maimamu hao waliwashutumu viongozi walioitisha mkutano huo chini ya Baraza hilo kuwa wanatumiwa na serikali kuwagonganisha Waislamu.

Kiongozi wa Al-Mallid Alhaj Said Rico alisema katika mkutano huo kuwa Waislamu wamefanywa mshumaa ambapo huhitajika muda maalum kwa shida fulani.

"Suala la Kadhi ni ajenda ya serikali na nyie mnatumiwa kufanikisha ajenda hiyo", alisema kiongozi huyo maarufu wa kikundi cha mhadhara jijini.

Naye Sheikh Yusuf Mikidadi akiwahoji viongozi hao alisema iweje Kardinali Pengo achaguliwe kwa taratibu za Kikatoliki bila ya kupeleka ombi serikalini wakati ambapo Waislamu kumpata kiongozi wao mpaka wapitie serikalini.

Aidha, alisema kwa kuwa mfumo wa kadhi ulikuwepo huko nyuma viongozi hao walipaswa kuhoji serikali kwa nini iliufuta.

Akizungumza kwa utulivu Sheikh Rashid Kadege wa Ubungo Darajani alisema Baraza hilo la Maimamu limeundwa kwa ujanja ili kukabili Shura ya Maimamu.

"Chombo tunachokitambua ni Shura ya Maimamu inayoongozwa na Sheikh Juma Mbukuzi", alisisitiza Sheikh huyo.

Aidha, Sheikh Kadege aliwataka Maimamu kutoliunga mkono Baraza hilo kwa madai kuwa ni chombo kilichoundwa na serikali.

"Nyie jana mlikuwa Ikulu mmemuomba Rais apige marufuku mihahara ni umoja gani mnaotaka chini ya Baraza lenu", alisema Sheikh Kadege na kuongeza kuwa baadhi ya viongozi wa Baraza hilo ndiyo waliohusika kukabidhi Msikiti wa Mwembechai kwa serikali na vile vile kuwafungia wanawake katika Msikiti wa Manyema ambako baadaye walivamiwa na kupigwa na polisi.

Baraza la Maimamu linaundwa na Masheikh ambao Waislamu wamekuwa wakiwatuhumu kutumiwa na serikali dhidi ya Waislamu.

Masheikh hao ni pamoja na Sheikh Hamid Jongo wa Msikiti wa Manyema, Sheikh Suleiman Kilemile wa Msikiti wa Tandika na Sheikh Alhadi wa Msikiti wa Temeke Mwisho.

Wengine ni pamoja na Katibu wa Baraza hilo Sheikh Mohammed Mtulia, Sheikh Mohammed Khalfan Rukara na Sheikh Hanzuruni Mungula.

Akielezea kuundwa kwa Baraza hilo Sheikh Hanzuruni Mungula alisema awali walimuona Makamu wa Rais Dk. Omar Ali Juma ambaye aliwapa "baraka" zake.
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook