CCM wilaya ya Morogoro imedaiwa kupora kiwanja Kitalu U mtaa wa Sabasaba mjini humo ambacho ni mali ya Umoja wa Wanawake wa Kiislamu.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka mkoani humo uporaji huo umeandamana na ufunguzi wa tawi la chama hicho na uuzaji wa viwanja vya biashara kwa watu mbalimbali.
Taarifa hizo zimedai kuwa CCM imeuza kila kiwanja kwa shilingi 50,000 ambapo kati ya hizo shilingi 30,000 kwa ajili ya kuimarisha chama hicho na shilingi 20,000 ufunguzi wa tawi.
Mpaka hivi sasa imedaiwa viwanja 10 vimeshatolewa kwa wafanyabiashara hao na ujenzi wa vibanda umeshaanza.
Kwa mujibu wa msemaji wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu, CCM imepora kiwanja baada ya Manispaa kuiandikia barua Jumuiya hiyo kusimamisha ujenzi wa uwigo (fance) ulioanza siku chache kabla.
Barua hiyo yenye Kumb. namba MGC/583/26 iliyoandikwa tarehe 17/9/1999 na kusainiwa na Bwana Mohammed Mkupete kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa iliitaka Jumuiya ya akina mama wa Kiislamu kusimamisha ujenzi wa uwigo kwa kuwa kiwanja hicho kilikuwa kwenye mgogoro.
Msemaji huyo alisema barua hiyo ya Manispaa iliwafikia wakati wakiwa na hati miliki ya eneo hilo iliyotolewa pia na ofisi hiyo ya Manispaa.
Alisema hati hiyo miliki walikabidhiwa kwa barua Kumb. namba MG/LD/8842/4 iliyotolewa Aprili 22, 1992.
Aidha, ruhusa ya kuanza ujenzi ilitolewa tarehe 14/7/1992 kwa barua Kumb. namba OP/MK/NS/MG/92.
Kabla ya hapo Jumuiya hiyo ilithibitishwa umiliki wa eneo hilo lililopo mtaa wa Sabasaba kwa barua Kumb. namba 4011/2/3/4 ya tarehe 31/12/1987.
CCM katika kadhia hiyo imedaiwa kuongozwa na Katibu wake wa wilaya Bwana Hussein Hading'oka.
Jitihada za gazeti hili kuwapata wasemaji wa CCM na Manispaa ya Morogoro ofisi ya ardhi na mipango miji hazikufanikiwa.
Ofisi ya CCM wilaya ilidai isingeweza kuzungumza na mtu yeyote jana baada ya taarifa za kifo cha Mwalimu Julius Nyerere.
Nako Manispaa AN-NUUR iliambiwa ofisa ardhi mipango mji hakuwepo hivyo ofisi hiyo isingeweza kusema lolote.
Wakati huo huo, Waislamu mjini Morogoro wamejiandaa kuvunja vibanda vya biashara na tawi la CCM lililojengwa katika kiwanja cha akina mama Kitalu U mtaa wa Sabasaba.
Hatua hiyo inafuatia baada ya kile kilichoeleza na waumini hao kuwa ni njama za kutaka kuteka nyara kiwanja hicho zinazofanywa na CCM kwa kutumia ofisi ya Manispaa.
Waumini hao wametishia kuwa iwapo haki haitatendeka katika suala hilo huenda amani ikawa hatarini.
"CCM imekuwa ikiendesha propaganda kuwa sisi tunatumiwa na vyama vya upinzani, wakati wao ndio waliovamia eneo letu, hatutishiki kwa hilo na tutasimama kidete kupigania haki yetu", amesema kijana mmoja wa Kiislamu mkazi wa Manzese mjini humo.
Jumuiya ya wanawake wa Kiislamu ambayo ndiyo wamiliki wa kiwanja hicho inaongozwa na Bibi Khadija Swedi ambaye ni Mwenyekiti na Katibu wake ni Bibi Mwanaidi Nasibu.
Wajumbe wa Jumuiya hiyo ni
pamoja na Mama Ramla Daudi, Mama Mtui na Bi Jamila Abdallah.
--
|
|