ILI mwanadamu aweze kuishi na kizazi chake kiendelee anahitaji vitu vinavyoitwa virutubisho. Virutubisho hivyo vinapatikana katika vyakula tunavyokula kila siku. Virutubisho vyote hivyo vinaweza kugawanywa katika makundi makubwa matatu. Makundi hayo ni virutubisho vya kutia nguvu na joto mwilini, virutubisho vya kujenga mwili na virutubisho vya kulinda mwili. Makala hii inatazama virutubisho vya kujenga mwili.
Virutubisho vya kujenga mwili kwa kiasi kikubwa ni protini. Hata hivyo, virutubisho vingine vinasaidia kwa kiasi fulani. Kama vile mafuta, maji na madini mbalimbali (chuma, na kadhalika).
Kila binadamu anahitaji virutubisho vya kujenga mwili. Hii ni kwa sababu, mimba na watoto wachanga ili waweze kukua lazima wapate virutubisho hivyo. Pia chembe chembe hai (cells) zinazoufanya mwili uwe kama tunavyouona zinahitaji virutubisho hivyo.
Damu, maji maji (machozi na kadhalika) na vitu vingine mwilini vinatengenezwa kwa kutumia virutubisho vya kujenga mwili. Kinga ya mwili pia inategemea sana kujengwa kutokana na vyakula vya kujenga mwili vikishirikiana na vile vya kulinda mwili.
Kwa hiyo, ndugu wananchi tujitahidi sana kula vyakula vya kujenga mwili ili tupate virutubisho vya kujenga mwili. Vyakula vya kujenga mwili ni kama vile nyama, samaki, maziwa, maharage, kunde, choroko, njegere, karanga na kadhalika.
Watoto, kina mama wajawazito
na wale wanaonyonyesha lazima wale kiasi cha kutosha cha vyakula vya kujenga
mwili. Vile vile kina mama wanaopata siku zao lazima wale vyakula hivyo
kiasi cha kutosha ili kufidia virutubisho vinavyopotea kila mwezi.
--
|
|