Ukosefu wa Dizeli waleta adha Mtwara
 
NAULI ya usafiri ndani ya mikoa ya Kusini imeongezeka mara dufu wakati bei ya korosho imeshuka kwa kiwango hicho hicho.

Hali hiyo imetokana na uhaba mkubwa wa dizeli ulioikumba sehemu hiyo.

"Kilo ya korosho iliyokuwa ikiuzwa shilingi 800 wiki mbili zilizopita, hivi sasa huuzwa kwa shilingi 450", amesema mfanyabiashara mmoja anayenunua korosho huko.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, mkazi mmoja wa Mtwara mjini amesema kuwa nauli kwenda Masasi hadi Mtwara imepanda hadi shilingi 4,500 toka shilingi 2000.

Aidha, alisema kuwa nauli ya kwenda Lindi imekuwa shilingi 3000 badala ya 1500.

Mkazi huyo Bw. Jaafar ameeleza kuwa tatizo la uhaba wa dizeli na mafuta ya taa limedumu kwa wiki mbili sasa.

Amesema kuwa uhaba huo kwa upande mmoja ni matokeo ya biashara huria ambapo wasambazaji wa bidhaa hiyo huangalia sehemu zenye maslahi makubwa zaidi.

Hata hivyo, imeelezwa kuwa mvua zilizonyesha ndizo zilizosababisha upungufu wa hivi sasa.

Malori yaliyokuwa yakifuata mafuta Dar es Salaam yalikwama njiani.

Kwa hali hii ni wafanyabiashara wachache wanaokwenda kuwekeza mikoa ya kusini.

Alipokuwa ziarani mikoa ya kusini hivi karibuni, Rais Mkapa ametoa matumaini kuwa tatizo la usafiri litaondoka hivi karibuni.

Alisema, mashirika mengi ikiwemo Kuwait Fund yameonesha nia ya kusaidia ujenzi wa barabara hiyo.

Hivi sasa ujenzi wa daraja la Nangurukuru katika mto Rufiji unaendelea kwa kasi.

Tatizo sugu la usafiri limekuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya wananchi wa Mtwara na Lindi.

Katika nyakati kadhaa, mikoa hiyo imekuwa ikitengwa na sehemu nyingine za nchi kutokana na ubovu wa barabara.

--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook