Wasakeni wauaji wenyewe - Ponda


WAISLAMU nchini wametakiwa kulinda uhai wao wenyewe iwapo serikali imekataa kutumia sheria zilizopo katika suala la Mwembechai.

Aidha, wametakiwa waitumie siku ya Mashahidi wa Mwembechai kutafakari la kufanya iwapo sheria za nchi bado zitakuwa hazijachukuwa mkondo wake.

Akiongea kufuatia majibu ya Rais Mkapa kwa madai ya Waislamu Sheikh Ponda amesema "Kama hakuna sheria, inakuwa ni jukumu la wananchi kujilinda na kujitetea wenyewe".

Kuhusu siku ya Februari 13, amewataka Waislamu wajiandae kuwakumbuka Mashahidi kwa namna ambayo itausaidia Uislamu katika siku zijazo.

Amesema siku hiyo programu maalum ifanyike kuwakumbusha Waislamu juu ya dhima waliyonayo kulinda na kutetea haki yao ya uhai kwa mujibu wa Qur'an.

Katika barua yake kwa Amir wa Shura ya Maimamu na Mwenyekiti wa Islamic Club, Sheikh Ponda amewaomba viongozi hao kuhakikisha kuwa Februari 13, 2000 inakuwa siku ya kihistoria nchini.

"Kama ilivyokuwa siku ya kihistoria Februari 13, 1998, Februari 13, 2000 ni lazima iwe ya kihistoria pia", alisema Sheikh Ponda Issa Ponda.

"Waislamu waliuliwa Februari 13 bila ya hatia, ni miaka miwili sasa serikali haitaki kutekeleza sheria zake yenyewe kuwahukumu wahusika, tutakuwa ni watu wa ajabu sana kama tutairidhia hali hii", aliongeza Sheikh Ponda ambaye ni Katibu wa Kamati ya Kutetea Haki za Waislamu nchini.

"Tunataka mtukusanyie umati mara kumi zaidi ya ule uliokuwepo Diamond Jubilee wakati wa Baraza la Idd na mtueleze lipi tufanye katika hali hii ya udhalimu usiojali hata haki yetu ya uhai", amesema Sheikh Ponda.

Kwa upande mwingine Sheikh Ponda amewataka Waislamu popote walipo wajiandae kwa siku hiyo.

"Kila mtu ajiandae kwa nauli yake, masurufu yake na ya kuwaachia watu wake, atakapolazimika kutoka kuitikia wito wa Februari 13", amesema Sheikh Ponda katika nasaha zake kwa Waislamu.

"Maadhali serikali inaelekea kuwahifadhi waliomwaga damu zetu bila ya haki, hatuna budi kujitoa muhanga kujihami wenyewe", amesema Sheikh Ponda na kuongeza, "yanayotokea Chechnya ni matokeo ya hali hii tuliyonayo hapa Waislamu kudhaniwa wao ni watu wa kukandamizwa wasio na hata haki ya uhai".

"Waislamu wasiozidi 5000 wanapambana na jeshi la watu laki moja (100,000) lenye silaha kali kwa sababu ya kutetea na kulinda haki yao ya uhai na uhuru wa kubaki Waislamu", amesema.

Wito wa Sheikh Ponda umeungana na msititizo alioutoa mwanasheria maarufu nchini na aliyekuwa mkuu wa chuo cha maafisa wa polisi Bwana Said El-Maamry kuhusiana na suala la Mwembechai.

Akizungumza katika Baraza la Iddi lililofanyika Diamond Jubilee Jumapili iliyopita, mwanasheria huyo aliwataka Waislamu waendelee kudai haki ya kuchunguza mauaji ya Mwembechai.

Bwana El-Maamry alisema kisheria linapotokea tukio, vifo visivyo vya kawaida au mtu kufia mikononi mwa polisi hutumika Inquest Ordinance kuhoji suala hilo.

Alisema wao kama wanasheria walishamuandikia Mwanasheria Mkuu kumtaka ufanyike uchunguzi kuhusiana na mauaji ya Mwembechai hata hivyo alisema katika hali iliyowashangaza Mwanasheria Mkuu hajawajibu hadi hii leo.

"Waislamu tusiliache suala la Mwembechai, tulisimamie mpaka tuone hatima yake", alimaliza kwa msisitizo mwanasheria huyo.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook