Mwembechai si suala la wahuni, ni Waislamu
KUWAITA wahanga na waathirika wa kadhia
ya Mwembechai wahuni, ni sawa na kuwaita Waislamu wote wahuni.
Hili ni suala la Waislamu wote na ndio maana limekuwepo katika madai ya Waislamu kwa Rais.
Balozi Abbas Sykes, ameeleza hayo akifafanua juu ya propaganda inayopigwa kulivua suala la Mwembechai na Waislamu.
Akizungumza na Waislamu katika Baraza la Eid, Balozi Sykes amesema, aliyewasilisha madai kwa Rais haikuwa Kamati ya Madabida wala yale hayakuwa madai ya Kamati. Yale yalikuwa madai ya Waislamu na ile ilikuwa Kamati ya Waislamu, alisema Balozi Sykes.
Alisema wenye madai yao ni umati uliokuwa umefurika Diamond Jubilee. Hivyo iwapo Mhe. Rais anadai suala la Mwembechai sio la Waislamu basi ni sawa na kuwaambia Waislamu pamoja na Masharifu waliohudhuria sio Waislamu.
Pamoja na Masheikh wakubwa kama Sharif Juneid, Sheikh Nurdeen Hussein, Sheikh Kilemile, Baraza la hilo la Eid lilihudhuriwa pia na Mawaziri Waislamu, Wabunge na baadhi ya Mabalozi.
Wakati huo huo, Balozi Abbas Sykes amewataka Waislamu kuimarisha umoja kama silaha muhimu ya kujiletea ukombozi na heshima.
Aidha, balozi Sykes amehimiza utekelezaji baada ya mazungumzo ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.
Akiongea katika Baraza la Eid wiki iliyopita, Balozi Sykes amesema, Dar es Salaam ina Waislamu milioni mbili kati ya wakazi wasiopungua milioni tatu. Lau wote watashikamana kwa hali na mali watafanya mambo makubwa sana, alisema.
Kuhusu umati mkubwa uliohudhuria Baraza hilo amesema, hajapata kuona umati mkubwa wa aina hiyo kwa muda mrefu.
"Nimefarijika sana baada ya kuona ukumbi huu sijapata kuona umati wa aina hii kwa muda mrefu", alisema Balozi Sykes na kuongeza, "Umoja ndio silaha kuu".
Balozi Abbas Sykes ni Mwenyekiti wa Dar es Salaam Islamic Club ambayo iliandaa Baraza la Eid kutoa ripoti ya majibu ya Rais kwa madai ya Waislamu.
Huko Mwanza, Waislamu wamemuambia Rais Mkapa, madai ya Waislamu juu ya dhulma hayatakoma hadi haki itendeke.
Aidha, wamesema suala la OIC litaendelea kupiganiwa kwani hapana sababu zozote za msingi za kuifanya Tanzania kutojiunga na jumuiya hiyo.
Akiwasilisha salamu hizo za Waislamu kwa Rais kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Sheikh Idrissa Sharif amesema hata ipite miaka 40 bado Waislamu wataendelea kudai suala la Mwembechai.
Sheikh Idrisa, ambaye ni Mwenyekiti wa Bakwata wa Mkoa amesema maadhali serikali imeruhusu ubalozi wa Vatican kuwepo nchini hakuna sababu ya kuikataa OIC.
Akizipokea salamu hizo Mkuu wa Mkoa Bw. Steven Mashishanga aliomba apewe salamu hizo kwa maandishi na atazifikisha kwa Rais.
Bw. Mashishanga alikuwa mgeni rasmi katika Baraza la Idd lililofanyika shule ya sekondari Thaqafa.
Ni katika hafla hiyo, Waislamu walitoa salamu zao kwa Rais.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |