Na Dkt. Abdallah J. Saffari (Wakili)
BAADA ya kusambaratika kwa sera na himaya ya Urusi mbabe pekee wa kweli duniani amebaki kuwa Mmarekani. Takriban mataifa yote ukiachia Libya, Cuba, China, Iraq na Iran yako chini ya makucha ya Wamarekani. Hivyo Umoja wa Mataifa na asasi zake zote navyo havikunusurika na mfumbato huu. Maana yake Umoja huo utaingilia kutatua ile migogoro ambayo Marekani (pengine na sahiba zake) wana maslahi yao tu, wala sio vinginevyo. Labda tujikumbushe kwa muhtsari kwani maslahi makubwa ya Marekani ni nini?
KILA mtu anajua kuwa Marekani ni kinara wa ubepari tangu kumalizika kwa vita vya pili vya dunia, Mhmili wa ubepari na unyonyaji katika kila sekta. Minghairi na sera hizo ni ujamaa na Uislamu.
Itikadi ya ujamaa ilipinga unyonyaji na kutaka kuimarisha hali nzuri kw awote katika nchi zilizofuata siasa hiyo wakati huo zikiongozwa na Urusi. Mafanikio na matatizo ya ujamaa yameandikiwa matopa kwa matopa ya vitabu kama vile ilivyo kwa matatizo na mafanikio ya ubepari. Tangu hapo hakuna lisilo na kasoro! Ila hapa ni muhimu kuelewa kuwa daima Marekani ilikuwa inatafuta mbinu ya kuzivunja sera za kijamaa.
Ndiyo maana baada ya kusambatarika kwa Urusi, serikali ya nchi hiyo ikanadi hadharani kwamba sasa hasimu yao ni Uislamu. Kuna majina kadhaa wa kadhaa yanayotumika kuhusu Uislamu kama vile siasa kali na magaidi wa Kiislamu. Hapa nyumbani kwetu Tanzania jina maarufu ni Mujahidina!
Lakini, iweje ubepari unaoongozwa na Wamarekani waone Uislamu ndiyo hasimu wake mkubwa kuliko wote duniani? Kwa uchache wa wasaa tutazigusia sababu kuu mbili. Kwanza, Uislamu unapinga riba ambayo ndiyo kitovu cha faida ya ubepari. Lazima dunia ikiri, pamoja na serikali ya Tanzania, kwamba leo hii riba ndiyo moja ya sababu kuu za mzigo wa madeni ya taifa hili.
Bila riba hakuna ubepari wa aina ambayo sote tunaufahamu ambao umeleta madhira na vifo kote hasa katika "dunia ya tatu". Ndiyo maana benki za nchi za Kiislamu za kweli hazitozi riba kwa maana ambayo inaeleweka na mataifa ya Magharibi. Sababu ya pili ni kuwa Uislamu wa kweli unapinga dhuluma. Imeshaandikwa mara nyingi katika tahariri za makala ya gazeti la AN-NUUR kwamba kwa Muislamu wa kweli, kukataa kuonewa sio nadhari (yaani hiari) bali ni ibada. Maana Qur'an inawaamuru Waislamu kutetea haki zao na kupingwa dhulma kwa njia tatu kuu.
Kwanza kujitoa muhanga kwa kupigana hata ikibidi kupoteza maisha. Pili, kukemea dhuluma popote pale duniani. Tatu, kuichukia dhulma na uonevu. Lakini hii ya tatu ndiyo ya mwisho kwa wale ambao ni dhoofu hali.
Lila na fila havitangamani. Hivyo ubepari wa Magharibi hauwezi kwa sanjari ya Uislamu. Na mifano ya mafanikio ya hali bora kwa raia wa nchi zinazofuata mafunzo ya Kiislamu ndiyo inazidi kuwatia hofu mabepari.
Yote haya maana yake nini? Ni kuwa taifa la watu wa aina hii hawana hofu na wako radhi kujitoa muhanga kama sehemu ya ibada yao. Sio rahisi kuwashinda watu kama hao.
Wanaweza kushindwa kwa muda, lakini uhasama na mgogoro utabaki pale mpaka kile ambacho wanadai kuwa ni haki yao kipatikane. Bila ya kushabikia mauaji ya hivi sasa nchini Algeria lakini bado huo ni mfano hai.
Baada ya chama cha Kiislamu kuporwa ushindi katika matokeo ya uchaguzi huru na halali wa miaka ya awali ya tisini nchini Algeria, jeshi lilibatilisha matokeo ya uchaguzi huo. Lakushangaza ni kuwa pamoja na dhulma hiyo ya wazi, hakuna hata taifa moja kati ya yale yanayojinadi kuwa vinara wa demokrasia walioikemea serikali ya kijeshi ambayo kwa makusudi kabisa iliwapora wananchi wa Algeria uongozi wao ambao waliuchagua kwa ridhaa yao wenyewe.
Matokeo yake hivi sasa Rais Abdelaziz Bouteflika amerithi kazi ngumu ya kujaribu kurejesha amani katika nchi ambayo ilikuwa "kisiwa cha amani" pengine kuliko nchi zote hapa Afrika.
Au ni vyema zaidi tuangalie mchango wa Uislamu katika harakati za ukombozi barani Afrika hususan Msumbiji na Tanganyika na kiasi fulani Rwanda.
Imeelezwa mara nyingi na wasomi wanahistoria kwamba wazee halwatan wa Dar es Salaam ambao walitoa mchango mkubwa katika kugombea uhuru wa Tanganyika. Akina Abdulwahid Sykes, Dosa Aziz, Sheikh Takadir, Jumbe Tambaza, Ali Sykes, Abbas Sykes kwa kuwataja wachache tu, walianzisha cheche za kupigana na ukoloni wa Kiingereza hata kabla ya Mwalimu Nyerere hajakanyaga Dar es Salaam.
Lakini, bila kujali kuwa yeye alikuwa Mkatoliki, wakamkaribisha na kumpa uongozi wa kugombea uhuru Tanganyika. Jambo hili muhimu katika historia ya nchi hii amelikiri Mwalimu Nyerere katika siku zake za mwisho wa uhai wake. Wakati Misikiti ilikuwa vituvu vya harakati za uhuru wa Tanganyika dini nyingine kubwa ziliwaeleza waumini wake wajitanibu na kumng'oa Mwingereza.
Na kule Msumbiji mambo hayakuwa tofauti. Mara nyingi Rais wa kwanza wa nchi hiyo, marehemu Samora Machel aligombana na hata kuwatimua nchini baadhi ya viongozi wa Kanisa Katoliki kwa madai kuwa walidumaza harakati za ukombozi wa nchi hiyo kisiasa na kiuchumi.
Zaidi ya yote miaka ya tisini tu huko Rwanda maelfu ya Wahutu walikimbilia katika Kanisa moja kujisalimisha kuuawa. Kwa mastaajabu ya kanisa hilo aliruhusu raia hao wasio na hatia kuuawa ndani ya kanisa. Hivi sasa mkuu huyo wa kanisa anasubiri mashtaka katika mauaji ya kukusudia.
Katika mazingira kama haya sio kweli kwamba Wamarekani wanapenda kuwatetea Waislamu wanaoangamizwa na yeyote yule na popote pale duniani. Mifano tumekwishaitoa. Ndiyo maana Wamarekani kuwakemea Warusi waache kuipiga Chechnya ni sawa na machozi ya mamba anayemtafuna binadamu. Katika vita hivi Warusi wanawapiga vita Waislamu ambao ndio hasimu mkuu wa Marekani.
Hitimisho
Vita vinavyoendelea Chechnya vinatupa mafunzo kadhaa na kuweza kutoa mapendekezo ya namna ya kuvimaliza. Kwanza hapana shaka mataifa yote makubwa hupenda, kwa visingizio mbalimbali, kuyavamia mataifa madogo. Itakumbukwa mnamo miaka ya sabini Urusi iliivamia Chekoslovakia.
Marekani ndiyo kinara wa maonevu hayo kwa kuzingatia vita vya Cambodia, Vietnam, Panama, Cuba na orodha haimaliziki.
Waingereza hadi leo wana mzozo na Argentina kuhusu visiwa vya Falklands baada ya vita vyao vikali vya miaka ya thamanini.
Wajerumani wanaeleweka kwa kusababisha vita mbili kuu za dunia. Na ni hivi karibuni tu Japan imeacha ubabe wa kuzivamia nchi jirani ikiwemo China kwa kuhofia kuwa bila shaka China ya sasa sio ya zamani.
Hata China nayo iliivamia Vietnman mnamo mwaka 1978 na hivi karibuni tu ilitaka kuichapa Taiwan. Katika hali kama hii hakuna taifa kubwa ambalo ni safi kabisa katika suala la uvamizi dhidi ya mataifa madogo au hata majimbo yao wenyewe. Kwa hiyo sio rahisi mataifa haya, kwa uhakika kabisa, kuweza kuyaasa mataifa mengine kuacha uvamizi na maangamizi.
Tumeshuhudia punde tu kuwa tayari Urusi imewasuta Marekani waache kuitetea Chechnya (kwa maneno matupu) wakati ambapo wenyewe ndiyo vinara wa uvamizi kote duniani. Pamoja na yote hayo lazima tuendelee kujifunza kuwa vita huweza kuleta ushindi wa bandia, sio kutatua mgogoro unaohusika. Mighairi yake huongeza chuki kwa aliyeshindwa ambayo hurindima mithili ya volcano na kuripuka kwa maangamizi makubwa baadaye.
Mifano iko mingi lakini wa haraka ni ule ushindi wa Israel dhidi ya nchi za Kiarabu katika vita vya miaka ya sitini. Ushindi huo "bandia" uliiwezesha Israel kuiteka na kuikalia milima ya Golan ambayo ni sehemu ya Syria kwa mujibu wa sheria zote za kimataifa. Hadi leo nchi hizo ni mahasimu wakubwa na mara kwa mara hukaribia kudundana tena.
Vita vya Falklands ni mfano mwingine. Hadi leo Argentina inadai kuwa visiwa hivyo ni sehemu yake. Madai hayo yanaungwa mkono na nchi nyingi pamoja na Cuba.
Pengine mfano mkubwa kupita yote ni kuwa hadi leo Wajerumani na Waingereza hawapikiki chungu kimoja kutokana na maangamizi ya vita vya pili vya dunia.
Kwa hiyo basi inawezekana kabisa Urusi ikauteka na kuukalia mji mkuu wa Chechnya, Grozny, kama wanavyoupania. Lakini ushindi huo utakuwa bandia maana maelfu kwa malaki ya ndugu wa askari watakaouawa na majeshi ya Urusi katika kulinda hadhi ya taifa lao dogo, utamaduni na dini yao, wataungana tena siku isiyo na jina na kudai haki yao kwa mbinu na nguvu mpya zaidi.
Enzi za amani kuletwa na ncha ya upanga zimegura. Vita ni hatua ya mwisho ya kuleta amani baada ya njia zote nyingine kuu kushindwa. Njia hizo yaani upatanishi, usuluhishi, majadiliano ndiyo huleta ushindi na amani ya kweli.
Urusi imezikwepa njia hizo kwa kuamini itapata ushindi wa chee ambao hadi leo bado wanautapia. Ni upuuzi kuamini kuwa mgogoro huo wa zaidi ya karne mbili unaweza kupatiwa ufumbuzi kwa mizinga ya helkopta na vifaru.
Kwa kuhitimisha tunajifunza pia namna serikali za mataifa madogo (pamoja na Tanzania) zinavyoweza kufumbia macho dhuluma hii dhidi ya Chechnya. Lakini ukiona mwenzako ananyolewa, tia maji. Na daima silaha ya mnyonge ni umoja!
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |