BARUA

Hii ni mbinu ya kutugawa

Ndugu Mhariri

Naomba nafasi katika gazeti letu la AN-NUUR nipate kutoa mawazo yangu.

Siku ya Jumaatu vyombo vya habari viliibuka na mchezo ulioshangiliwa sana na wapinzani, mchezo huo ulichukua vichwa vikubwa vikubwa katika kurasa za mwanzo (Front pages) juu ya Sheikh Mbukuzi na Rais Mkapa kukutanishwa na Dk. Omar Ali Juma nyumbani kwake katika chakula kilichohudhuriwa na baadhi ya viongozi wengine wa serikali.

Kwa uhalisi wake harakati za Waislamu hapa nchini sasa hivi zimefikia hatua ya kuridhisha kidogo, hali inayoonesha harufu ya muungano na umoja katika jamii ya Kiislamu, hasa hasa tukio la Jumapili la Waislamu kukutana pamoja na kuonesha hisia zao pale Diamond Jubilee katika sikukuu ya Idil-Fitr.

Swali la kujiuliza ni hili kwanini vyombo vya habari ambavyo asilimia kubwa ama ni vya kanisa au hupendelea watu wa mrengo wa kushoto vimeshabikia suala la Sheikh Mbukuzi kula chakula na kukutanishwa na Rais Mkapa!

Hivi kulikoni hasa vyombo hivyo vyote havikugusia hata kidogo siku hiyo tukio la Diamond Jubilee ambalo ndilo la msingi kwetu sisi Waislamu.

Hivi kwanini hasa mtangazaji wa Radio One na BBC, amesikika BBC asubuhi ya Jumatatu akipeperusha hoja za Waislamu za Diamon Jubilee na wala hakusikika hata kidogo katika Radio One!

Hii inaonekana ni mbinu kali iliyopangwa na kusimamiwa na makachero wa serikali ili Amiri aonekane na kashfa hii inayowachukiza Waislamu tugawanyike na kuanza upya baada ya maandalizi yetu yaliyochukua takriban miaka miwili na zaidi.

Siyo siri tukio hili limeishaleta mitizamo tofauti tofauti katika jamii ya Kiislamu kwani ukipita sehemu mbalimbali unakuta mjadala ni huo.

Mimi kama mimi naona bado mabo hayajaharibika ikiwa tumeweza kuyagundua haya kwani historia ya harakati za Waislamu hapa nchini inadhihirisha kwamba nguvu ya Waislamu huvunjwa vunjwa na umoja wao kusambaratishwa na kukatishwa tamaa pale mkono wa serikali unapopenyeza na kuingilia sehemu nyeti ya uongozi wa Waislamu pindi kunapotokea hali yakutokuwa makini dhidi ya maadui.

Munawar Mussa,
Morogoro.


Dk. Salmin mbona unatukanganya

Ndugu Mhariri

NINGEPENDA kuanza kwa kuweka wazi kwamba, tatizo la muda mrefu la mwezi mwandamo wa kuanza na kwisha kwa Ramadhani hapa nchini si la kimaumbile na wala si la kidini bali ni la kisiasa.

Iwapo BAKWATA ambalo ni chombo kilichoanzishwa na mwanasiasa aliyeongoza nchi hii katika serikali ya awamu ya kwanza, litaondolewa mamlaka ya kutangaza mwezi, naamini, ufumbuzi wa tatizo hilo utapatikana kwa urahisi kabisa.

Lakini Mamufti wa serikali wakiachiwa waendelee na ukiritimba wa maamuzi juu ya suala hilo, nina mashaka kuwa tatizo hilo litabaki kama lilivyo. Watu wanaoliendekeza Baraza hilo lisilo na ridhaa ya waumini wataendelea kutenda dhambi ya kula mchana wa Ramadhani na kufunga siku ya Eid.

Sheria za nchi mojawapo kati ya hizi katu haziathiri mwandamo wa mwezi. Shreia hizo zinafanyakazi ndani ya mipaka ya nchi hizo lakini mwezi kama lilivyojua hauna mipaka ya utaifa.

Kauli ya Mheshimiwa Rais wa Zanzibar aliyoitoa katika Baraza la Id kwamba Mtume ni wetu wote lakini Saudia ina sheria zake hivyo hatuwezi kufuata tangazo la kuandama kwa mwezi la nchi hiyo kwa kweli inajipinga kimantiki na kutukanganya.

Nijuavyo ni kuwa Waislamu wote ulimwenguni ni umma mmoja au tuseme wafuasi wa Mtume Muhammad (s.a.w.) ambaye ndiye aliyetumwa na Mwenyezi Mungu atuhimiza kufunga na kufungua saumu kwa kufuata mwezi punde tu unapoandama.

Hivyo, Waislamu wote tunapaswa kufuata agizo hilo bila kuzingatia mipaka ya utaifa. Mwezi ukionekana Saudia, Tanzania, Vaticani, Somalia na kwingineko Waislamu wote waufuate.

Ni kwa sababu hiyo, wale wanaofunga na kufungua wasikiapo mwezi umeandama Saudia, si kwamba wanafuata amri za mfalme Fahd au Msaudia yeyote, bali Fahd au Msaudia mwingine yeyote anaweza tu kutoa taarifa za kuandama kwa mwezi.

Kama Saudi Arabia ingekulikuwa na mwezi wake bandia hapo tungelazimika kutofautiana nayo lakini madamu nchi hiyo haina mbingu peke yake basi hakuna sababu ya kula mchana na kufunga siku ya Idi kwa kisingizio cha kutouona mwezi wa Tanzania.

Enzi za Mtume (s.a.w.) Waislamu wa nchi moja walipishana siku au masiku na Waislamu wa nchi nyingine kwa sababu ya tatizo la mawasiliano. Kama wangelikuwa na teknolojia ya mawasiliano tuliyonayo hivi leo wangefunga na kufungua pamoja. Ni ajabu sisi kutofautiana siku mbili ilihali tuna vyombo vya mawasiliano vya papo kwa hapo.

Tukiendelea kutazama mwezi kwa mipaka ya utaifa, ushauri wa Rais Salmin Amour kuwa Masheikh na wanazuoni watafute ufumbuzi wa tatizo la sala tatu za Idi zilizojitokeza mwaka huu ni dhahiri hautotekelezeka.

Kama nilivyokwisha sema tatizo la mwezi linasababishwa na ukiritimba wa maamuzi wa chombo kinachomilikiwa na serikali kutokana na hali hiyo, siku ya kuanza kufunga na siku ya Idd zinategemea "baraka" za viongozi wa chombo hicho na si kuandama kwa mwezi.

Ni wazi kupitia BAKWATA kuna mkono wa maadui unaofanya jitihada za makusudi kuwafarakanisha Waislamu kwa tatizo hilo. Lengo ni kuwakosesha Waislamu umoja na mshikamano na badala yake wapoteze wakati wao muhimu kulumbana na hata kuhasimiana juu ya suala hilo.

Kwa bahati nzuri Waislamu wameng'amua njama hiyo na hivyo kudhibiti hali ya mambo. Ndio maana Waislamu safari hii wameona ni muhimu kuandaa Baraza moja la Iddi ili kuwa na nguvu na sauti moja.

Batuli Hussein,
Morogoro.



Masjid Mtoro chagueni viongozi bora

Ndugu Mhariri

NAOMBA nafasi kidogo katika gazeti lako tukufu nitoe yangu machache.

Kwanza napenda niwakumbushe Waislamu wenzangu wote hususan wamumini wa Msikiti wa Mtoro wajitahidi wachague viongozi bora na waadilifu ambao watakuwa mstari wa mbele katika kupigania dini ya Mwenyezi Mungu na wawe wanaharakati katika kuwakomboa Waislamu na Uislamu.

Pia musikubali kuchaguliwa kiongozi asiyekubalika na waumini na musikubali mtu ajipachike madaraka kwamba yeye ndiye kiongozi wa Misikiti wakati hafai kabisa.

Jumanne bin Mussa Tetele,
Dar es Salaam.


Ni wajibu waumini kuzungumzia siasa

Ndugu Mhariri

WAUMINI wa dini Misikitini na Makanisani wanafundishwa kuwa dhulma ni dhambi na lazima wapambane kwa nadharia na vitendo kuondosha udhalimu mahala popote pale.

Kwa mantiki hiyo, kama viongozi wa serikali ya CCM hawatendi haki, ni wajibu kwa waumini kutumia mimbari na madhabahu kuwakemea viongozi hao. Si vibaya kutumia fursa za Misikitini na Makanisani kujadili namna ya kuwawajibisha na hata kuwang'oa madarakani.

Mara nyingi Maaskofu wamekuwa wakitekeleza wajibu huo na mfano wa karibuni ni ule wa Askofu Shayo wa Zanzibar. Askofu huyo alitumia fursa yake ya kidini kuishambulia serikali.

Inashangaza kuwa, Masheikh pamoja na kukwepa kuikemea serikali bado shutuma zinaelekzwa Misikitini kwamba inatumiwa kwa masuala ya kisiasa.

Dk. Salmin Amour badala ya kumkemea Askofu Shayo, yeye ameelekeza shutuma kwa Waislamu wanaochanganya dini na siasa.

Napenda kuwatanabaisha viongozi wote wa serikali kuwa, waumini wanalazimika kuchanganya dini na siasa ili kuondoa udhalimu kama Mungu alivyoagiza.

Habiba Swaleh,
Kibaha, Pwani.



Waislamu hawana haki katika Tanzania

Ndugu Mhariri

AKUTUKANAYE hakuchagulii tusi msemo huu umethibitika hasa kutokana na kauli ya Rais Mkapa kwa kile alichokisema majibu ya madai ya Waislamu.

Waislamu turejee pale Mhe. Mkapa aliposema waliohusika pale Mwembechai si Waislamu. Hebu Waislamu kila mmoja ajiulize na ajione yeye kuwa si Muislamu sababu waliopigwa Msikitini ni Waislamu iweje leo Rais aseme si Waislamu. Kwa maana wanaopatikana Misikitini si Waislamu (wahuni) sasa hili ni tusi.

Waislamu turejee majibu aliyoyatoa Rais kwa makini kisha tukae kama kikundi na baadaye kundi hilo litoe majibu, na pia Waislamu kila mmoja wetu ajiandae na kupambana na lolote litakalotokea InshaAllah.

Dongo Msimbe,
Morogoro.



Ndege wote walie akilia bundi kasheshe

Ndugu Mhariri

NAOMBA unipe japo nafasi kidogo tu katika gazeti letu tukufu la AN-NUUR ili nami nipate kuungana na Waislamu wenzangu duniani katika kukosoa maovu yanayoendeshwa waziwazi na baadhi ya mataifa.

Kwa ufupi tu tuelekee kule Chechnya ambapo Waislamu wenzetu wanauawa kila kukicha. Sasa swali la kujiuliza ni hivi:

Hivi hili Baraza la Umoja wa Mataifa wanangoja nini kuikemea Russia kuacha mara moja kuua watu hovyo?

Je, ingekuwa ni Wakristo wanauliwa namna hiyo wasingeingilia kati? Ukweli ni kwamba hakuna hata baadhi ya Marais wanaolaani kitendo hicho. Ila madomo yao yameelekea kwenye Mapinduzi ya Ivory Coast.

Sasa hili ni Baraza gani la Umoja wa Mataifa ambalo linabagua nchi, watu na dini zao?

Al-Jaan Juma,
Dar es Salaam.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook