Demokrasia duniani
Na Mbaraka Sharrifs

MAANA ya demokrasia ni uhuru wa watu kuchagua serikali yao. Itakayowaongoza kwa maslahi yao, na wao kuchaguliwa katika serikali hiyo. Ama kwa kupitia kwenye vyama au wagombea wa kujitegemea.

Demokrasia ni pamoja na uhuru wa kusema na kutoa mawazo yako, kukosoa jambo na kuunga mkono chochote ili mradi huvunji sheria. Kukutana na watu wengine, kufanya maandamano ya amani ili kuwasilisha hisia zako na kadhalika.

Baada ya kuanguka Ukomunisti na Muungano wa Kisovieti, hali ya siasa ilibadilika duniani. Huku tukishuhudia kuondoka vita baridi baina ya mataifa ya Ulaya.

Hatimaye mataifa ya Magharibi na Marekani yakichukua hatamu za uongozi duniani katika nyanja za uchumi, siasa, ulinzi na kadhalika.

Madola ya Magharibi yanatangaza demokrasia ya vyama vingi kwa kuzua suala la haki za binadamu. Vyama vingi ni sharti mojawapo la misaada na mikopo kutoka vyombo vya fedha vya kimataifa na nchi wahisani.

Lakini demokrasia sio bidhaa inayotoka nchi moja kwenda nchi nyingine. Bila kuangalia hali halisi ya nchi inayohusika. Mataifa ya Magharibi yamepata upinzani mkali katika suala hili.

Imethibitika kwamba mataifa ya Magharibi kutangaza haki za binadamu ni unafiki mkubwa. Sababu katika nchi kama Marekani haki za binadamu haziheshimiwi, ubaguzi wa rangi bado upo. Vyama vya kibaguzi kama K.K.K vinazidi kuimarika. Katika kuonea watu weusi, polisi na mahakama za Marekani hazitendi haki saa kwa raia wote bila kujali rangi zao.

Raia wasiokuwa weupe wanakandamizwa, leo Wamarekani weupe na weusi wanaishi katika dunia mbili tofauti.

Fujo zilizotokea mwezi Mei, 1992 katika mji wa Los Angeles mji wa pili mkubwa wa Marekani na kuenea tena katika majimbo mengine ishirini. Ghasia hizo zilianza baada ya mahakama ya Simi Valley ya Jiji la Los Angeles kutoa hukumu ya kutodhibiti kosa kwa askari polisi wanne weupe waliompiga marungu Mmarekani mwenye asili ya Afrika Bw. Rodney King.

Alipigwa marungu 56 kwa sekunde 81 na askari hao weupe. Kanda ya video ilitolewa kama ushahidi, lakini ilionekana askari hawana hatia.

Kufuatia hukumu hiyo watu weusi walitia moto maduka, majumba, magari na ofisi za serikali (kumbuka Mwembechai). Mwisho wa fujo za Los Angeles watu 40 walikufa, 2000 walijeruhiwa na wengine 3500 wakatiwa mbaroni na kuacha hasara ya dola bilioni moja. Ilibidi kuweka askari 5000 ili kudhibiti hali hiyo.

Hiyo ndiyo nchi inayotetea haki za binadamu au demokrasia, utawala bora na uhuru kwa wote. Wala haihitaji elimu ya Chuo Kikuu kujua kuwa huo ni unafiki dhahiri, huo ni mfano mmoja tu kuonesha unafiki wao. Ipo mingi inayotendwa na nchi hizo.

Turudi kwenye hoja za nchi za Magharibi zimeshindwa kukubali demokrasia ya kweli pale Waislamu wanaposhinda uchaguzi. Uchaguzi ulio huru na haki. Mifano ya Algeria na Misri inatosha kuthibitisha hayo. Jeshi katika Algeria lilipofuta uchaguzi huru, serikali za magharibi zilikaa kimya.

Katika hali kama hiyo, tunashauri Waislamu kuweka mbele maslahi ya dini yao na baadaye ndio kifuate chama. Maana imeonekana siasa hizi si za uadilifu, ili tukiunge mkono chama chochote ni lazima maslahi na haki zetu zitekelezwe. Vinginevyo tuachane navyo vyama vya matapeli wa siasa za wachumia tumbo.

Katika hali hiyo kama CCM ilipongeza serikali kwa kuua watu pale Mwembechai basi Waislamu, tuungane kuilaani kwa kudhulumu damu za Waislamu wale watiifu katika hili itikadi ya chama isiwepo. Hoja yetu ni Waislamu wameuawa.

Katika hili nampongea mbunge wa Kigamboni Mhe. Kitwana Kondo kwa kuelewa kwa kina mipaka ya siasa na wajibu wake katika maslahi ya Uislamu naomba wengine waige hili.

Sheikh Mbukuzi anapodai haki za Waislamu inabidi aungwe mkono na Waislamu wote Tanzania bila kujali vyama vyetu, maana Sheikh Mbukuzi anadai haki za Uislamu, hafanyi kampeni ya chama chochote. Kwa hiyo wewe hata kama ni mkereketwa lazima ushiriki hili kwa ajili ya Uislamu wako.

Kama Mbunge wa CCM, NCCR, CHADEMA waliukebehi Uislamu bungeni ni lazima. Waislamu waungane bila kujali vyama kuhoji uhalali wa wabunge wale kutoa lugha mbovu dhidi ya Uislamu na Waislamu. Hoja hapa si kumtetea Kapuya, hapa ni Uislamu umekashifiwa.

Hiyo ndiyo maana ya demokrasia sio kutetea vyama vyenu na kuukana Uislamu wenu.

Sheikh Muhamed al Ghazal mtaalam wa Harakati za Uislamu kutoka Chuo Kikuu cha Constantine Algeria anasema: "Waislamu ni wenye kujijua na kujitambua na kuuthamini Uislamu wao mbele ya itikadi yoyote ile".

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook