Madai ya Waislamu yako pale pale - Sheikh Mbukuzi


AMIR wa Shura ya Maimamu amesema kupeana mkono na Rais Benjamin Mkapa si ishara kumalizika matatizo ya Waislamu kwa serikali.

Amir Mbukuzi amesema matatizo hayo yataondoka iwapo serikali itashughulikia malalamiko na kero za Wananchi kiadilifu.

Akihutubia Waumini katika Msikiti wa Ubungo darajani juzi, Sheikh Mbukuzi alisema ipo mifano mingi ya mahasimu kushikana mikono na kisha baada ya hapo kila mmoja kuondoka na msimamo wake.

Huku akifuatishwa kwa Takbira, Sheikh Mbukuzi alitaja mifano hiyo kuwa ni pamoja na ule wa Kiongozi wa Palestina kushikana mkono na viongozi wa Israil lakini bado mapambano baina ya mataifa hayo yakizidi kuuma.

Sheikh Mbukuzi aliwaambia waumini waliokuwa wakimsikiliza kuwa pamoja na tukio hilo au lile kupewa mialiko na viongozi bado madai ya Waislamu yako pale pale kuwa serikali haiwatendei haki Waislamu.

Aliwataka Waislamu kujiepusha na njama za watu wanaotaka kuwagawa ili ikosekane nguvu ya pamoja katika kupigania haki zao za kidini na kijamii.

Aidha alilaumu mtindo wa baadhi ya Waislamu kushutumu wenzao bila ya kwanza kufanya uchunguzi au kuwahoji wahusika.

Katika sherehe ya Id mosi mwaka huu makamu wa Rais Dk. Omar Ali Juma aliandaa chakula ambapo alialika wageni mbalimbali wakiwemo masheikh na viongozi wa juu wa serikali.

Maakuli hayo yalihudhuriwa pia na Rais Benjamin Mkapa na Waziri mkuu Frederick Sumaye ambaye siku hiyo alivalia kanzu na kofia.

Sheikh Juma Mbukuzi alikuwa miongoni mwa Masheikh waliopata mualiko katika hafla hiyo fupi iliyofanyika asubuhi mara baada ya swala ya Id.

Akiongea na gazeti hili jioni ya siku iliyofuata, Sheikh Mbukuzi pamoja na mambo mengine alieleza kuwa mualiko wake aliupata kupitia kwa bwana Hanzuruni Mungula.

Alisema kuwa baada ya kuswali Id alipigiwa simu na bwana huyo akimtaka waonane katika msikiti wa Jamia Kinondoni .

Sheikh alisema alipofika katika msikiti huo bwana Mungula alimwambia kuwa alipewa mualiko na Dk. Omar ambao alipaswa kuufikisha mapema hata hivyo hakuweza kufanya hivyo.

Kwa hiyo ilikuwa hapana budi wawasiliane haraka kwani shughuli yenyewe iliandaliwa kufanyika asubuhi ile hivyo pamoja na taarifa hizo kuchelewa alimuomba waongozane muda huo kuelekea kwenye nyumbani kwa makamu.

Aliendelea kueleza Sheikh kuwa walipofika nyumbani kwa Dk. Omar walikuta waalikwa wengi wakiwemo masheikh maarufu, mawaziri na viongozi wa juu wa nchi.

Kiongozi wa shughuli hiyo alimtaja kuwa alikuwa Imamu wa msikiti mmoja ulioko maeneo ya Upanga jijini ambao ni maarufu kwa mawaziri na maafisa waislamu.

Kuhusiana na tukio la kushikana mkono na Rais Mkapa, Sheikh alieleza kuwa wakati shughuli ikielekea ukingoni, aliitwa na bwana Mungula wakati Rais akielekea kwenye gari.

"Mara nikasikia sauti ya makamu wa Rais ikimtaka Mungula aniambie niharakishe ili tusalimiane na Rais", Sheikh Mbukuzi alisema.

Aliendelea kueleza kuwa walipofika jirani na Rais, makamu wa Rais ndiye aliyehusika kuwatambulisha na mara picha zikachukuliwa.

"Hatukuongea zaidi na Rais mbali ya kusalimiana kwa kushikana mikono", alisema kwa msisitizo Amir Mbukuzi.

Aidha alikanusha taarifa za baadhi ya magazeti kuwa katika masalimiano hayo alisikika akisema kuwa kuanzia hapo matatizo ya Waislamu na serikali yamekwisha.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook