MASHAIRI


CCM

Tukisema CCM, bado kiboko ya vyama,
Bado mwatushutum, hamtaki kuungana,
Mbunge sasa Azim, Premji wa Kigoma,
Si kila Chama ni Chama, Chama baba CCM.

Said M. Nyoka (Udogo si hoja),
UHURU Des. 1999.

CCM 'chokoraa'

CCM kuwa baba, wa vyama vyote nchini,
Hayo ni mawazo haba, na utashi wa maoni,
Sema bingwa wa kuiba, kura zao wapinzani,
Wa vyama vyote nchini, CCM sio Baba.

Mfumo wa vyama vingi, upo kote duniani,
Bali watawala wengi, kwenye bara hili duni,
Wamezidia vigingi, wanaongoza kwa khani,
Ndipo nasema nchini, CCM sio Baba.

Mfano zile chaguzi, za mitaa majimboni,
Zilijaa uchafuzi, hila zenu wajivuni,
Mnatamba waziwazi, ajabu pasipo soni,
Natongoa ubaini, CCM sio Baba.

Heri ungesema TAA, na Baba ungeliwini,
TANU mwana ujamaa, huyo mtoto baini,
CCM “Chokoraa”, kijukuu namba wani,
Cha kawaida nchini, CCM sio Baba.

Ubaba hapo uwapi, majahili na wahuni,
Msitulambishe pipi, kwa lugha yenu laini,
Mola hamumuogopi, enyi waja kulikoni?
Kaditamati nchini, CCM sio Baba.

Mweta S. Mweta (Ugali moto mboga moto),
Tandika kwa Kipua,
S.L.P. 455,
Dar es Salaam.


Mkapa amepatia

Mkapa amepatia, wala si wa kulaumu,
Sisi tuliojifia, ndio tulo madhulumu,
Ajabu kutegemea, yeye vyema kuhukumu,
Ya Mkapa malimwengu, Chui kuhukumu Mbuzi!

Mkapa amepatia, kinyume asingeweza,
Wenzetu kutuulia, ilikuwa ni lazima,
Ya Luambano kadhia, ni chambo walimtuma,
Ya Mkapa malimwengu, Chui kuhukumu Mbuzi!

Mkapa amepatia, amesema ukweli,
Mola keshatuambia, ndo mkweli wa kauli,
Hawa wanatuchukia, na hizo ndizo dalili,
Ya Mkapa malimwengu, Chui kuhukumu Mbuzi!

Mkapa amepatia, alisema hadharani,
Kauli tumesikia, na kusoma gazetini,
Ndio ya kwao tabia, kututusi waumini,
Ya Mkapa malimwengu, Chui kuhukumu Mbuzi!

Mkapa amepatia, hiyo ndiyo mila yao,
Usoni kutuchekea, chuki vifuani mwao,
Ajabu Islamia, kuwategemea hao,
Ya Mkapa malimwengu, Chui kuhukumu Mbuzi!

Mkapa amepatia, jambo kaliweka wazi,
Khatima limefikia, keshatoa utatuzi,
Ni sisi kufikiria, wa kufanya uamuzi,
Ya Mkapa malimwengu, Chui kuhukumu Mbuzi!

Mkapa amepatia, yake ameshamaliza,
Hajali la kutukia, hayuko wa kumuweza,
Islamu si raia, haki wameshapoteza,
Ya Mkapa malimwengu, Chui kuhukumu Mbuzi!

Mkapa amepatia, kusapoti waloua,
Nami siwezi kulia, majibu niliyajua,
Dhalimu wa njema nia, sijawahi kumjua,
Ya Mkapa malimwengu, Chui kuhukumu Mbuzi!

Mkapa amepatia, “hongera” Rais mwema,
Salamu twakutumia, kwa yako kubwa “huruma”,
“Wahuni” twakuambia, umetutendea “wema”,
Ya Mkapa malimwengu, Chui kuhukumu Mbuzi!

Saballa J.R.
Box 347,
Shinyanga.


Kutumiwa sitotaka

Nakataa katakata, mimi na Bakwata hata,
Ukiniunga nakata, sikubali kuambata,
Kuwa nao si kupata, ni pabaya kujikita,
Mimi na Bakwata hata, kutumiwa sitotaka.

Bakwata yake matata, yanazibomoa kuta,
Si yao laini hata, kuwa wa kuwafuata,
Sitaki hata kwa vita, shauri nimeshakata,
Mimi na Bakwata hata, kutumiwa sitotaka.

Kutumika kama kata, mtungini kwenda chota,
Kisha kuzua sakata, na lawama kuzileta,
Katu hawatonipata, sing’oki wakinivuta,
Mimi na Bakwata hata, kutumiwa sitotaka.

Mipaka waliyokata, mimi sintowafuata,
Nachelea kuja juta, kushika yao sirata,
Kale nilishajifuta, dini ya kwendeshwa puta,
Mimi na Bakwata hata, kutumiwa sitotaka.

Hata kwa cheo kupata, na ahadi ya kitita,
Aje Shekhe kuniita, nipate kuwafuata,
Bado moyo utasita, kamwe hautotakata,
Mimi na Bakwata hata, kutumiwa sitotaka.

Hawa watu wa matata, wenye kutaka kupata,
Dunia kuikamata, ndicho wanachokitafuta,
Kamba wamekatakata, kinyume wanatuita,
Mimi na Bakwata hata, kutumiwa sitotaka.

Witiri nakana hata, njia nilishafuata,
Nyingine si ya Bakwata, wao hawatonipata,
Dini sichezi karata, najua cha kufuata,
Mimi na Bakwata hata, kutumiwa sitotaka.

Jihad R. Saballa,
Box 347,
Shinyanga.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook